12
Nathani Amkemea Daudi
1 Bwana akamtuma Nathani kwa Daudi. Alipofika kwake akamwambia, “Katika mji mmoja kulikuwepo na watu wawili, mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa maskini. 2 Yule mtu tajiri alikuwa na idadi kubwa sana ya kondoo na ngʼombe, 3 lakini yule maskini hakuwa na chochote ila kondoo jike mdogo aliyekuwa amemnunua. Akamtunza kondoo huyo, akakulia kwake pamoja na watoto wake. Kondoo huyo alishiriki chakula cha bwana wake na kunywea kikombe chake hata pia huyo kondoo alilala mikononi mwa bwana wake. Kwake alikuwa kama binti yake.
4 “Siku moja yule tajiri akafikiwa na mgeni, lakini huyo tajiri akaacha kuchukua mmoja wa kondoo au ngʼombe wake mwenyewe amwandalie mgeni. Badala yake akachukua yule kondoo jike mdogo aliyekuwa mali ya yule maskini na kumwandalia yule mgeni wake.”
5 Daudi akawakwa na hasira dhidi ya mtu huyo tajiri na kumwambia Nathani, “Hakika kama Bwana aishivyo, mtu huyo aliyefanya hivyo anastahili kufa! 6 Lazima alipe mara nne zaidi, kwa ajili ya kondoo huyo, kwa sababu amefanya jambo kama hilo na hakuwa na huruma.”
7 Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli. 8 Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba ya Israeli na Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi. 9 Kwa nini ulilidharau neno la Bwana kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria, Mhiti kwa upanga na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni. 10 Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria, Mhiti kuwa mkeo.’
11 “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Kutoka kwa nyumba yako mwenyewe nitaleta maafa juu yako. Mbele ya macho yako mwenyewe nitatwaa wake zako na kumpa yeye aliye wa karibu nawe, naye atakutana kimwili na wake zako mchana mwangavu. 12 Ulifanya kwa siri, lakini nitalifanya jambo hili wakati wa mchana mwangavu mbele ya Israeli yote.’ ”
13 Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Bwana.”
Nathani akamjibu, “Bwana amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. 14 Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za Bwana kuonyesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.”
15 Baada ya Nathani kurudi nyumbani kwake, Bwana akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua. 16 Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha. 17 Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao.
18 Kunako siku ya saba yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Wakati mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.”
19 Daudi akaona kuwa watumishi wake wananongʼonezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?”
Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.”
20 Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya Bwana, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani kwake kwa kutaka kwake, wakamwandalia chakula, naye akala.
21 Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.”
22 Akajibu, “Wakati mtoto alipokuwa bado yungali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? Bwana aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’ 23 Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”
24 Ndipo Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake akakutana naye kimwili. Akazaa mwana, wakamwita jina lake Solomoni. Bwana alimpenda Solomoni. 25 Kwa kuwa Bwana alimpenda, akatuma neno kwa Daudi kwa kinywa cha nabii Nathani kuwa mtoto aitwe Yedidia* Yedidia maana yake Apendwaye na Bwana. kwa ajili ya Bwana.
26 Wakati huo Yoabu akapigana dhidi ya Raba jamii ya Waamoni na kuteka ngome la kifalme. 27 Kisha Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi, kusema, “Nimepigana dhidi ya Raba, nami nimetwaa chanzo chake cha maji. 28 Sasa kusanya vikosi vilivyobaki na ukauzingire mji kwa jeshi na kuuteka. La sivyo, nitauteka mimi, nao utaitwa kwa jina langu.”
29 Kwa hiyo Daudi akakusanya jeshi lote akaenda Raba, akaushambulia na kuuteka. 30 Akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu,† Talanta moja ya dhahabu ni sawa na kilo 34. nayo ilizungushiwa vito vya thamani. Ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo. 31 Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka, naye akawaweka kwenye kazi ya kutengeneza matofali. Akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.