7
Hekima
Afadhali sifa nzuri kuliko manukato safi,
nayo siku ya kufa kuliko ya kuzaliwa.
Afadhali kwenda kwenye nyumba ya msiba
kuliko kwenda kwenye nyumba ya karamu,
kwa kuwa kifo ni hatima ya kila mwanadamu,
imewapasa walio hai kuliweka hili mioyoni mwao.
Huzuni ni afadhali kuliko kicheko,
kwa sababu uso wenye huzuni wafaa kwa moyo.
Moyo wa wenye hekima uko katika nyumba ya msiba,
lakini moyo wa wapumbavu uko katika nyumba ya anasa.
Afadhali kusikia karipio la mtu mwenye hekima,
kuliko kusikiliza wimbo wa wapumbavu.
Kama ilivyo kuvunjika kwa miiba chini ya sufuria,
ndivyo kilivyo kicheko cha wapumbavu.
Hili nalo pia ni ubatili.
 
Dhuluma humfanya mtu mwenye hekima kuwa mpumbavu,
nayo rushwa huuharibu moyo.
 
Mwisho wa jambo ni bora kuliko mwanzo wake,
uvumilivu ni bora kuliko kiburi.
Usiwe mwepesi kukasirika rohoni mwako,
kwa kuwa hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.
 
10 Usiseme, “Kwa nini siku za kale zilikuwa bora kuliko siku hizi?”
Kwa maana si hekima kuuliza maswali kama hayo.
 
11 Hekima, kama ulivyo urithi, ni kitu chema
na huwafaidia wale walionalo jua.
12 Hekima ni ulinzi kama fedha ilivyo ulinzi,
lakini faida ya maarifa ni hii:
kwamba hekima huhifadhi maisha ya aliye nayo.
13 Tafakari kile Mungu alichokitenda:
Nani awezaye kunyoosha
kile ambacho yeye amekipinda?
14 Nyakati zikiwa nzuri, ufurahi,
lakini nyakati zikiwa mbaya, tafakari:
Mungu amefanya hiyo moja,
naam, sanjari* Sanjari hapa maana yake mwandamano wa vitu, wanyama au watu. na hiyo nyingine.
Kwa hiyo, mwanadamu hawezi kugundua
kitu chochote kuhusu maisha yake ya baadaye.
15 Katika maisha haya yangu ya ubatili nimeshaona haya mawili:
mtu mwadilifu akiangamia katika uadilifu wake,
naye mtu mwovu akiishi maisha marefu katika uovu wake.
16 Usiwe mwenye haki kupita kiasi,
wala usiwe na hekima kupita kiasi:
kwa nini kujiangamiza mwenyewe?
17 Usiwe mwovu kupita kiasi,
wala usiwe mpumbavu:
kwa nini kufa kabla ya wakati wako?
18 Ni vyema kushika hilo moja
na wala usiache hilo jingine likupite.
Mtu amchaye Mungu ataepuka huko kupita kiasi. Au: atafuata hayo yote mawili.
 
19 Hekima humfanya yeye aliye nayo kuwa na uwezo zaidi
kuliko watawala kumi katika mji.
 
20 Hakuna mtu mwenye haki duniani
ambaye hufanya mambo ya haki
na kamwe asitende dhambi.
 
21 Usitie maanani kila neno linalosemwa na watu,
la sivyo, waweza kumsikia
mtumishi wako akikulaani:
22 kwa kuwa unafahamu moyoni mwako
kwamba wewe mwenyewe mara nyingi
umewalaani wengine.
23 Yote haya niliyajaribu kwa hekima, nikasema,
“Nimeamua kuwa na hekima”:
lakini hii ilikuwa nje ya uwezo wangu.
24 Vyovyote hekima ilivyo,
hekima iko mbali sana na imejificha,
ni nani awezaye kuigundua?
25 Nikageuza fikira zangu ili kuelewa,
kuchunguza na kuitafuta hekima
na kusudi la mambo,
na ili kuelewa ujinga wa uovu,
na wazimu wa upumbavu.
 
26 Nimeona jambo lililo chungu kuliko mauti,
mwanamke ambaye ni mtego,
ambaye moyo wake ni wavu wa kutegea
na mikono yake ni minyororo.
Mtu ampendezaye Mungu atamkwepa,
bali mwenye dhambi atanaswa naye.
27 Mhubiri anasema, “Tazama, hili ndilo nililogundua:
“Nimegundua kitu kimoja baada ya kingine nilipokuwa katika kusudi la mambo:
28 ningali natafiti
lakini sipati:
nilimpata mwanaume mmoja mnyofu miongoni mwa elfu,
lakini hakuna mwanamke mmoja mnyofu miongoni mwao.
29 Hili ndilo peke yake nililolipata:
Mungu amemuumba mwanadamu mnyofu,
lakini mwanadamu amebuni mambo mengi.”
 

*7:14 Sanjari hapa maana yake mwandamano wa vitu, wanyama au watu.

7:18 Au: atafuata hayo yote mawili.