7
Hamani Aangikwa
1 Basi mfalme na Hamani wakaenda kula chakula pamoja na Malkia Esta. 2 Walipokuwa wakinywa mvinyo katika siku ya pili, mfalme akauliza tena, “Malkia Esta, ni nini haja yako? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.”
3 Kisha Malkia Esta akajibu, “Kama nimepata kibali kwako, ee mfalme, tena kama inapendeza utukufu wako, nijalie maisha yangu, hii ndiyo haja yangu. Pia uokoe watu wangu, hili ndilo ombi langu. 4 Kwa kuwa mimi na watu wangu tumeuzwa kwa kuangamizwa, kuchinjwa na kuharibiwa. Kama tungalikuwa tumeuzwa tu kuwa watumwa wa kiume na wa kike, ningalinyamaza kimya, kwa sababu shida kama hii isingalitosha kumsumbua mfalme.”
5 Mfalme Ahasuero akamuuliza Malkia Esta, “Ni nani huyu? Yuko wapi mtu huyu aliyethubutu kufanya jambo kama hili?”
6 Esta akasema, “Mtesi na adui ni huyu mwovu Hamani.”
Hamani alifadhaika mbele ya mfalme na malkia. 7 Mfalme akainuka kwa ghadhabu, akaacha mvinyo wake, akaenda kwenye bustani ya jumba la kifalme. Lakini Hamani, akitambua kwamba mfalme ameshaamua hatima yake, alibaki nyuma kumsihi Malkia Esta aokoe maisha yake.
8 Mara mfalme aliporudi kutoka bustani ya jumba la kifalme na kuja kwenye ukumbi wa karamu, Hamani alikuwa akijitupa juu ya kiti mahali ambapo Esta alikuwa akiegemea.
Mfalme akasema kwa nguvu, “Je, atamdhalilisha malkia hata huku nyumbani akiwa pamoja nami!”
Mara neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, walifunika uso wa Hamani. 9 Kisha Harbona, mmoja wa matowashi wanaomtumikia mfalme, akasema, “Mahali pa kuangika watu penye urefu wa mita ishirini na mbili pako nyumbani mwa Hamani. Alikuwa amepatengeneza kwa ajili ya Mordekai, ambaye alizungumza ili kumsaidia mfalme.”
Mfalme akasema, “Mwangikeni juu yake!” 10 Kwa hiyo wakamtundika Hamani mahali alipokuwa ameandaa kwa ajili ya Mordekai. Ndipo ghadhabu ya mfalme ikatulia.