6
1 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Sasa utaona kitu nitakachomfanyia Farao: Kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawaachia watu waende; kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.”
2 Pia Mungu akamwambia Mose, “Mimi ndimi Bwana. 3 Nilimtokea Abrahamu, Isaki na Yakobo kama Mungu Mwenyezi,* Mungu Mwenyezi hapa ni jina la Kiebrania, El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote). ingawa sikuwajulisha Jina langu, Yehova, Mimi mwenyewe sikujitambulisha kwao. 4 Pia niliweka Agano langu nao kuwapa nchi ya Kanaani, ambako waliishi kama wageni. 5 Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha huzuni cha Waisraeli ambao Wamisri wamewatia utumwani, nami nimelikumbuka Agano langu.
6 “Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi Bwana, nami nitawatoa mtoke katika kongwa la Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu. 7 Nitawatwaa mwe watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu, niliyewatoa chini ya kongwa la Wamisri. 8 Nami nitawaleta mpaka nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi Bwana.’ ”
9 Mose akawaarifu Waisraeli jambo hili, lakini hawakumsikiliza kwa sababu ya maumivu makuu ya moyoni na utumwa wa kikatili.
10 Ndipo Bwana akamwambia Mose, 11 “Nenda, mwambie Farao mfalme wa Misri awaachie Waisraeli waondoke nchini mwake.”
12 Lakini Mose akamwambia Bwana, “Ikiwa Waisraeli hawatanisikiliza, kwa nini yeye Farao anisikilize mimi, ambaye huzungumza kwa kigugumizi?”
Orodha Ya Jamaa Ya Mose Na Aroni
13 Ndipo Bwana akanena na Mose na Aroni kuhusu Waisraeli na Farao mfalme wa Misri, naye akawaamuru wawatoe Waisraeli kutoka Misri.
14 Hawa walikuwa wakuu wa jamaa zao:
Wana wa Reubeni mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli walikuwa Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi. Hawa walikuwa ndio koo za Reubeni.
15 Wana wa Simeoni walikuwa Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani. Hawa walikuwa ndio koo za Simeoni.
16 Haya ndiyo majina ya wana wa Lawi kufuatana na orodha zao: Gershoni, Kohathi na Merari. Lawi aliishi miaka 137.
17 Wana wa Gershoni kwa koo, walikuwa Libni na Shimei.
18 Wana wa Kohathi walikuwa Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Kohathi aliishi miaka 133.
19 Wana wa Merari walikuwa Mahli na Mushi.
Hizi ndizo zilizokuwa koo za Lawi kufuatana na orodha zao.
20 Amramu akamwoa Yokebedi, shangazi yake, ambaye alimzalia Aroni na Mose. Amramu aliishi miaka 137.
21 Wana wa Ishari walikuwa Kora, Nefegi na Zikri.
22 Wana wa Uzieli walikuwa Mishaeli, Elisafani na Sithri.
23 Aroni akamwoa Elisheba binti wa Aminadabu ndugu yake Nashoni, naye akamzalia Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari.
24 Wana wa Kora walikuwa Asiri, Elikana na Abiasafu. Hawa walikuwa ndio koo za Kora.
25 Eleazari mwana wa Aroni akamwoa mmoja wa binti za Putieli, naye akamzalia Finehasi.
Hawa walikuwa ndio wakuu wa jamaa za Walawi, ukoo kwa ukoo.
26 Hawa walikuwa Aroni na Mose wale wale ambao Bwana aliwaambia, “Watoeni Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.” 27 Ndio hao hao waliozungumza na Farao mfalme wa Misri kuhusu kuwatoa Waisraeli Misri. Ilikuwa ni huyo Mose na huyo Aroni.
Aroni Kuzungumza Badala Ya Mose
28 Bwana aliponena na Mose huko Misri, 29 akamwambia, “Mimi ndimi Bwana. Mwambie Farao mfalme wa Misri kila kitu nikuambiacho.”
30 Lakini Mose akamwambia Bwana, “Kwa kuwa mimi huzungumza kwa kigugumizi, Farao atanisikiliza mimi?”