24
Agano Lathibitishwa
1 Kisha Mungu akamwambia Mose, “Njooni huku juu kwa Bwana, wewe na Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli. Mniabudu kwa mbali, 2 lakini Mose peke yake ndiye atakayemkaribia Bwana; wengine wasije karibu. Nao watu wasije wakapanda pamoja naye.”
3 Mose alipokwenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za Bwana, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema Bwana tutakifanya.” 4 Ndipo Mose akaandika kila kitu Bwana alichokuwa amesema.
Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli. 5 Kisha akawatuma vijana wanaume wa Kiisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa Bwana. 6 Mose akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu. 7 Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema Bwana, nasi tutatii.”
8 Ndipo Mose akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo Bwana amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”
9 Mose na Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, 10 nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu. 11 Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa.
12 Bwana akamwambia Mose, “Panda uje kwangu huku mlimani na ukae hapa, nami nitakupa vibao vya mawe, vyenye sheria na amri ambazo nimeziandika ziwe mwongozo wao.”
13 Basi Mose akaondoka na Yoshua mtumishi wake, naye Mose akapanda juu kwenye mlima wa Mungu. 14 Mose akawaambia wazee wa Israeli, “Tungojeni hapa mpaka tutakapowarudia. Aroni na Huri wako pamoja nanyi, na kila aliye na neno aweza kuwaendea wao.”
15 Mose alipopanda juu mlimani, wingu liliufunika huo mlima, 16 nao utukufu wa Bwana ukatua juu ya Mlima Sinai. Kwa muda wa siku sita wingu lilifunika mlima, na siku ya saba Bwana akamwita Mose kutoka katikati ya lile wingu. 17 Kwa Waisraeli utukufu wa Bwana ulionekana kama moto uteketezao juu ya mlima. 18 Kisha Mose akaingia ndani ya lile wingu alivyokuwa akipanda mlimani. Naye akakaa huko mlimani kwa muda wa siku arobaini, usiku na mchana.