32
Ndama Wa Dhahabu
(Kumbukumbu 9:6-29)
1 Watu walipoona kuwa Mose amekawia sana kushuka kutoka mlimani, walimkusanyikia Aroni na kumwambia, “Njoo, tutengenezee miungu itakayotutangulia. Kwa maana huyu jamaa yetu Mose aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui jambo lililompata.”
2 Aroni akawajibu, “Vueni vipuli vya dhahabu ambavyo wake zenu, wana wenu na binti zenu wamevaa, mkaniletee.” 3 Kwa hiyo watu wote wakavua vipuli vyao, wakavileta kwa Aroni. 4 Akavichukua vile vitu walivyomkabidhi, akavifanyiza kwa kusubu sanamu yenye umbo la ndama, akaichonga kwa kutumia chombo. Kisha wakasema, “Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”
5 Aroni alipoona hili, akajenga madhabahu mbele ya yule ndama na kutangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa Bwana.” 6 Kwa hiyo siku iliyofuata watu wakaamka asubuhi na mapema na kutoa sadaka za kuteketeza na sadaka za amani. Baadaye watu wakaketi kula na kunywa, nao wakasimama, wakajizamisha katika sherehe.
7 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka. 8 Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kuyeyusha yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’ ”
9 Bwana akamwambia Mose, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu. 10 Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”
11 Lakini Mose akamsihi Bwana Mungu wake, akasema, “Ee Bwana, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu? 12 Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako. 13 Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote ambayo niliwaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ” 14 Kisha Bwana akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.
15 Mose akageuka, akashuka kutoka mlimani akiwa na vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake. Vilikuwa vimeandikwa pande zote mbili, mbele na nyuma. 16 Vibao hivyo vilikuwa kazi ya Mungu; maandishi yalikuwa mwandiko wa Mungu, yaliyochorwa kama muhuri juu ya vibao.
17 Yoshua aliposikia sauti za watu wakipiga kelele, akamwambia Mose, “Kuna sauti ya vita kambini.”
18 Mose akajibu:
“Si sauti ya ushindi,
wala si sauti ya kushindwa;
ni sauti ya kuimba ninayosikia.”
19 Mose alipoikaribia kambi na kuona yule ndama na ile michezo, hasira yake ikawaka, akatupa vile vibao vilivyokuwa mikononi mwake, akavipasua vipande vipande pale chini ya mlima. 20 Kisha akamchukua yule ndama waliokuwa wamemtengeneza na kumchoma kwenye moto, kisha akamsaga kuwa unga, akanyunyiza kwenye maji na kuwafanya Waisraeli wanywe.
21 Mose akamwambia Aroni, “Watu hawa walikufanyia nini, hata ukawaongoza kufanya dhambi kubwa hivyo?”
22 Aroni akamwambia, “Usikasirike bwana wangu. Unajua jinsi watu hawa walivyo tayari kwa maovu. 23 Wao waliniambia, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza. Kwa kuwa huyu jamaa yetu Mose aliyetupandisha kutoka Misri, hatufahamu yaliyompata.’ 24 Kwa hiyo nikawaambia, ‘Yeyote aliye na kito chochote cha dhahabu avue.’ Kisha wakanipa hiyo dhahabu, nami nikaitupa motoni, akatokea huyu ndama!”
25 Mose akaona kuwa watu wameasi, kwa kuwa Aroni alikuwa amewaacha waasi, na hivyo kuwa kichekesho kwa adui zao. 26 Kwa hiyo Mose akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Yeyote aliye upande wa Bwana, aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia.
27 Ndipo alipowaambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Kila mmoja wenu ajifunge upanga wake kiunoni aende huku na huko kambi yote mwisho hadi mwisho mwingine, kila mmoja amuue ndugu yake, na rafiki yake na jirani yake.’ ” 28 Walawi wakafanya kama Mose alivyoamuru, siku ile wakafa watu wapatao 3,000. 29 Kisha Mose akasema, “Leo mmewekwa wakfu kwa Bwana, kwa kuwa mlikuwa kinyume na wana wenu wenyewe na ndugu zenu, naye Mungu amewabariki leo.”
30 Siku iliyofuata Mose akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwa Bwana, labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”
31 Hivyo Mose akarudi kwa Bwana na kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu. 32 Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kwenye kitabu ulichoandika.”
33 Bwana akamjibu Mose, “Yeyote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kwenye kitabu changu. 34 Sasa nenda, uongoze hao watu mpaka mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”
35 Ndipo Bwana akawapiga watu kwa ugonjwa wa tauni kwa sababu ya yale waliyoyafanya kwa ndama yule ambaye alitengenezwa na Aroni.