13
Huduma Inayompendeza Mungu
1 Endeleeni kupendana kama ndugu. 2 Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua. 3 Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.
4 Ndoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,
“Kamwe sitakuacha,
wala sitakupungukia.”
6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,
“Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”
7 Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao. 8 Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele.
9 Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria. 10 Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake.
11 Kuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. 12 Vivyo hivyo, Yesu naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe. 13 Kwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba. 14 Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.
15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.
17 Watiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa hesabu. Watiini ili wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu.
18 Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia. 19 Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.
Maombi Ya Kuwatakia Baraka
20 Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya Agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Yesu, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, 21 awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni Pake, kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.
Maneno Ya Mwisho Na Salamu
22 Ndugu zangu, nawasihi mchukuliane na maneno yangu ya maonyo, kwa kuwa nimewaandikia waraka mfupi tu.
23 Nataka ninyi mjue kwamba ndugu yetu Timotheo amefunguliwa kutoka gerezani. Akifika mapema, nitakuja pamoja naye kuwaona.
24 Wasalimuni viongozi wenu wote na watakatifu wote. Wale wa kutoka Italia wanawasalimu.
25 Neema iwe nanyi nyote. Amen.