15
Elifazi Anaongea: Ayubu Anadhoofisha Imani
Kisha Elifazi Mtemani akajibu:
“Je, mtu mwenye hekima hujibu kwa mawazo matupu,
au kujaza tumbo lake kwa upepo wenye joto wa mashariki?
Je, aweza kubishana juu ya maneno yasiyofaa,
kwa hotuba zisizo na maana?
Lakini unadhoofisha hata uchaji wa Mungu
na kuzuia ibada mbele za Mungu.
Dhambi yako inasukuma kinywa chako,
nawe umechagua ulimi wa hila.
Kinywa chako mwenyewe kinakuhukumu, wala si changu;
midomo yako mwenyewe inashuhudia dhidi yako.
 
“Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa?
Ulizaliwa kabla ya vilima?
Je, wewe husikiliza mashauri ya siri ya Mungu?
Je, wewe unaizuia hekima iwe yako mwenyewe?
Wewe unajua kitu gani tusichokijua sisi?
Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi?
10 Wale wenye mvi na wazee wako upande wetu,
watu ambao ni wazee hata kuliko baba yako.
11 Je, faraja za Mungu hazikutoshi,
au maneno yaliyosemwa kwako kwa upole si kitu?
12 Kwa nini moyo wako unakudanganya,
na kwa nini macho yako yanangʼaa,
13 ili kwamba upate kutoa hasira yako dhidi ya Mungu,
na kumwaga maneno kama hayo kutoka kinywani mwako?
 
14 “Mwanadamu ni kitu gani, hata aweze kuwa safi,
au yeye aliyezaliwa na mwanamke, hata aweze kuwa mwadilifu?
15 Kama Mungu hawaamini watakatifu wake,
kama hata mbingu zenyewe si safi machoni pake,
16 sembuse mwanadamu ambaye ni mwovu na mpotovu,
ambaye hunywa uovu kama anywavyo maji!
 
17 “Nisikilize mimi nami nitakueleza,
acha nikuambie yale niliyoyaona,
18 ambayo watu wenye hekima wameyanena,
bila kuficha lolote walilopokea toka kwa baba zao
19 (wakati ambao wao peke yao ndio walipewa nchi,
hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao):
20 Mtu mwovu siku zake zote hupata mateso,
miaka yote aliwekewa mkorofi.
21 Sauti za kutisha hujaa masikioni mwake;
katika kufanikiwa kwake, wanyangʼanyi humshambulia.
22 Hukata tamaa kuokoka gizani;
amewekwa kwa ajili ya upanga.
23 Hutangatanga, akitafuta chakula;
anajua kwamba siku ya giza iko karibu.
24 Taabu na maumivu makuu vinamtia hofu;
humshinda kama mfalme aliye tayari kwa vita,
25 kwa sababu amemkunjia Mungu ngumi yake
na kujigamba dhidi ya Mwenyezi,
26 kwa kiburi akishambulia dhidi ya Mungu
akiwa na ngao nene, iliyo imara.
 
27 “Ingawa uso wake umefunikwa na mafuta kwa unene
na kiuno chake kimevimba kwa kunenepa,
28 ataishi katika miji ya magofu,
na katika nyumba ambazo haziishi mwanadamu yeyote,
nyumba zinazokuwa vifusi.
29 Hatatajirika tena, nao utajiri wake hautadumu,
wala mali zake hazitakuwa nyingi juu ya nchi.
30 Hatatoka gizani;
mwali wa moto utanyausha machipukizi yake,
nayo pumzi ya kinywa cha Mungu itamwondolea mbali.
31 Asijidanganye mwenyewe kutumainia ubatili,
kwa kuwa hatapata malipo yoyote.
32 Atakuwa amelipwa kikamilifu kabla ya wakati wake,
nayo matawi yake hayatastawi.
33 Atafanana na mzabibu uliopukutishwa matunda yake kabla hayajaiva,
kama mzeituni unaodondosha maua yake.
34 Kwa kuwa jamii ya wasiomcha Mungu watakuwa tasa,
nao moto utateketeza hema za wale wanaopenda rushwa.
35 Hutunga mimba ya madhara na kuzaa uovu;
matumbo yao huumba udanganyifu.”