25
Mwaka Wa Sabato
(Kumbukumbu 15:1-11)
1 Bwana akamwambia Mose katika Mlima Sinai, 2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapa ninyi, nchi yenyewe ni lazima ishike Sabato kwa ajili ya Bwana. 3 Kwa miaka sita mtapanda mazao katika mashamba yenu, nanyi kwa miaka sita mtaikata mizabibu yenu matawi na kuvuna mazao yake. 4 Lakini mwaka wa saba nchi lazima iwe na Sabato ya mapumziko, Sabato kwa Bwana. Msipande mbegu katika mashamba yenu, wala msikate mizabibu yenu matawi. 5 Msivune na kuweka akiba kinachoota chenyewe, wala kuvuna na kusindika zabibu ambayo hamkuhudumia mashamba yake. Nchi lazima iwe na mwaka wa mapumziko. 6 Chochote nchi itoacho katika mwaka wa Sabato kitakuwa chakula chenu wenyewe, watumishi wenu wa kiume na wa kike, mfanyakazi aliyeajiriwa, na mkazi wa muda anayeishi miongoni mwenu, 7 vilevile malisho ya mifugo yenu na wanyama pori katika nchi yenu. Chochote nchi itakachozalisha kinaweza kuliwa.
Mwaka Wa Yubile
8 “ ‘Hesabu Sabato saba za miaka, yaani miaka saba mara saba, ili Sabato saba za miaka utakuwa muda wa miaka arobaini na tisa. 9 Ndipo tarumbeta itapigwa kila mahali katika siku ya kumi ya mwezi wa saba. Katika Siku ya Upatanisho, piga tarumbeta katika nchi yako yote. 10 Mwaka wa hamsini mtauweka wakfu na kutangaza uhuru katika nchi kwa wakazi wake wote. Itakuwa ni yubile* Yubile ni baragumu iliopigwa kila mwaka wa hamsini; ni Sabato ya nchi ya kila mwaka wa hamsini uliokuwa mwaka wa ukombozi, yaani kuachia huru. kwenu; kila mmoja wenu atairudia mali ya jamaa yake, na kila mmoja kurudi kwenye ukoo wake. 11 Mwaka wa hamsini utakuwa yubile kwenu, msipande wala msivune kile kiotacho chenyewe, au kuvuna zabibu zisizohudumiwa. 12 Kwa kuwa ni yubile, nayo itakuwa takatifu kwenu; mtakula tu kile kilichotoka moja kwa moja mashambani.
13 “ ‘Katika huu Mwaka wa Yubile, kila mmoja atarudi kwenye mali yake mwenyewe.
14 “ ‘Ikiwa utauza ardhi kwa mmoja wa wazawa wa nchi yako, au ukinunua ardhi kutoka kwake, mmoja asimpunje mwingine. 15 Utanunua ardhi kwa mzawa wa nchi yako kwa misingi ya hesabu ya miaka baada ya Yubile. Naye ataiuza kwako kwa misingi ya hesabu ya miaka iliyobaki kwa kuvuna mavuno. 16 Miaka inapokuwa mingi, utaongeza bei, nayo miaka ikiwa michache, utapunguza bei, kwa sababu kile anachokuuzia kwa hakika ni hesabu ya mazao. 17 Mmoja asimpunje mwingine, bali utamcha Mungu wako. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
18 “ ‘Fuateni amri zangu, mwe waangalifu kutii amri zangu, nanyi mtaishi salama katika nchi. 19 Kisha nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba na kuishi humo kwa salama. 20 Mwaweza kuuliza, “Tutakula nini katika mwaka wa saba ikiwa hatutapanda wala kuvuna mazao yetu?” 21 Nitawapelekeeni baraka ya pekee katika mwaka wa sita, kwamba nchi itazalisha mazao ya kutosha kwa miaka mitatu. 22 Mnapopanda mwaka wa nane, mtakula mavuno ya miaka iliyopita. Pia mtaendelea kuyala mazao hayo hadi mvune mavuno ya mwaka wa tisa.
23 “ ‘Kamwe ardhi isiuzwe kwa mkataba wa kudumu, kwa sababu nchi ni mali yangu, nanyi ni wageni na wapangaji wangu. 24 Katika nchi yote mtakayoshika kuwa milki yenu, ni lazima mtoe ukombozi wa ardhi.
25 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini na akauza baadhi ya mali yake, ndugu yake wa karibu atakuja na kukomboa kile ndugu yako alichokiuza. 26 Iwapo mtu huyo hana jamaa wa karibu wa kukomboa mali hiyo kwa ajili yake, lakini yeye mwenyewe akafanikiwa na kupata mali itoshayo kuikomboa, 27 ataamua tena thamani yake kwa miaka tangu alipoiuza, na kurudisha kiasi kilichobaki cha thamani kwa mtu ambaye alikuwa amemuuzia mali hiyo, naye ataweza kuirudia mali yake. 28 Lakini kama hatapata njia ya kumlipa mnunuzi, ile mali aliyouza itabaki kumilikiwa na mnunuzi mpaka Mwaka wa Yubile. Mali hiyo itarudishwa mwaka wa Yubile, naye ataweza kuirudia mali yake.
29 “ ‘Ikiwa mtu atauza nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta, yeye anayo haki ya kuikomboa mwaka mzima baada ya mauzo ya hiyo nyumba. Wakati huo anaweza kuikomboa. 30 Ikiwa haikukombolewa kabla ya mwaka mmoja kamili kupita, nyumba iliyo ndani ya mji uliozungukwa kwa ukuta itakuwa mali ya kudumu ya mnunuzi na wazao wake. Haitarudishwa mwaka wa Yubile. 31 Lakini nyumba zilizo vijijini bila ya kuwa na kuta zilizozizunguka zitahesabiwa kama mashamba. Zinaweza kukombolewa, nazo zirudishwe katika mwaka wa Yubile.
32 “ ‘Walawi siku zote wana haki ya kukomboa nyumba zao katika miji ya Walawi wanayoimiliki. 33 Kwa hiyo mali ya Mlawi inaweza kukombolewa, yaani nyumba iliyouzwa katika mji wowote wanaoushikilia itarudishwa mwaka wa Yubile, kwa sababu nyumba zilizo katika miji ya Walawi ni mali yao miongoni mwa Waisraeli. 34 Lakini nchi ya malisho iliyo mali ya miji yao kamwe isiuzwe, ni milki yao ya kudumu.
35 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako. 36 Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako. 37 Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida. 38 Mimi ndimi Bwana Mungu wako, niliyekuleta kutoka nchi ya Misri nikupe nchi ya Kanaani, nami niwe Mungu wako.
39 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini katikati yako, naye akajiuza kwako, usimfanye atumike kama mtumwa. 40 Atatendewa kama mfanyakazi aliyeajiriwa, au kama mkazi wa muda katikati yako, naye atatumika mpaka Mwaka wa Yubile. 41 Ndipo yeye na watoto wake wataachiwa, naye atarudi kwa watu wa ukoo wake, na kwenye mali ya baba zake. 42 Kwa sababu Waisraeli ni watumishi wangu niliowaleta kutoka nchi ya Misri, kamwe wasiuzwe kama watumwa. 43 Usiwatawale kwa ukatili, lakini utamcha Mungu wako.
44 “ ‘Watumwa wako wa kiume na wa kike watatoka katika mataifa yanayokuzunguka; kutoka kwao waweza kununua watumwa. 45 Pia waweza kununua baadhi ya wakazi wa muda wanaoishi katikati yako, na jamaa ya koo zao waliozaliwa katika nchi yako, nao watakuwa mali yako. 46 Hao waweza kuwarithisha watoto wako kuwa urithi wao, na wanaweza kuwafanya watumwa maisha yao yote, lakini usiwatawale ndugu zako Waisraeli kwa ukatili.
47 “ ‘Ikiwa mgeni au mkazi wa muda katikati yako atakuwa tajiri, na mmoja wa wazawa wa nchi yako akawa maskini, naye akajiuza kwa yule mgeni anayeishi katikati yako, au kwa mmoja wa jamaa wa koo za wageni, 48 anayo haki ya kukombolewa baada ya kujiuza. Mmoja wa jamaa zake aweza kumkomboa: 49 Mjomba wake, au binamu yake, au yeyote aliye ndugu wa damu katika ukoo wake aweza kumkomboa. Au ikiwa atafanikiwa, anaweza kujikomboa mwenyewe. 50 Yeye na huyo aliyemnunua watahesabu muda kuanzia mwaka aliojiuza hadi Mwaka wa Yubile. Mahali pa kuanzia bei ya kuachiwa kwake itakadiriwa kwa ujira unaolipwa mfanyakazi aliyeajiriwa kwa idadi ya hiyo miaka. 51 Ikiwa imebaki miaka mingi, ni lazima atalipia ukombozi wake fungu kubwa la bei iliyolipwa kumnunua yeye. 52 Ikiwa miaka iliyobaki ni michache kufikia Mwaka wa Yubile, atafanya hesabu yake, naye atalipa malipo yanayostahili kwa ajili ya ukombozi wake. 53 Atatendewa kama mtu wa kuajiriwa mwaka hadi mwaka; lazima uone kwamba yule aliyemnunua hamtawali kwa ukatili.
54 “ ‘Hata ikiwa hakukombolewa kwa njia mojawapo ya hizi, yeye na watoto wake wataachiwa katika Mwaka wa Yubile, 55 kwa maana Waisraeli ni mali yangu kama watumishi. Wao ni watumishi wangu, niliowatoa kutoka nchi ya Misri. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
*25:10 Yubile ni baragumu iliopigwa kila mwaka wa hamsini; ni Sabato ya nchi ya kila mwaka wa hamsini uliokuwa mwaka wa ukombozi, yaani kuachia huru.