24
Kufufuka Kwa Yesu
(Mathayo 28:1-10; Marko 16:1-8; Yohana 20:1-10)
1 Mnamo siku ya kwanza ya juma, alfajiri na mapema, wale wanawake walichukua yale manukato waliyokuwa wameyaandaa, wakaenda kaburini. 2 Wakakuta lile jiwe limevingirishwa kutoka kwenye kaburi, 3 lakini walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. 4 Walipokuwa wanashangaa juu ya jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayongʼaa kama umeme wakasimama karibu nao. 5 Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao mpaka chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu? 6 Hayuko hapa; amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba: 7 ‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi na waovu ili asulubiwe, na siku ya tatu afufuke.’ ” 8 Ndipo wakayakumbuka maneno ya Yesu.
9 Waliporudi kutoka huko kaburini, wakawaeleza wale wanafunzi kumi na mmoja pamoja na wengine wote mambo haya yote. 10 Basi Maria Magdalene, Yoana, na Maria mama yake Yakobo, pamoja na wanawake wengine waliofuatana nao ndio waliwaelezea mitume habari hizi. 11 Lakini hawakuwasadiki hao wanawake, kwa sababu maneno yao yalionekana kama upuzi. 12 Hata hivyo, Petro akainuka na kukimbia kwenda kule kaburini. Alipoinama kuchungulia, akaona vile vitambaa vya kitani, ila hakuona kitu kingine. Naye akaenda zake akijiuliza nini kilichotokea.
Njiani Kwenda Emau
(Marko 16:12-13)
13 Ikawa siku iyo hiyo, wanafunzi wawili wa Yesu walikuwa njiani wakienda kijiji kilichoitwa Emau, yapata maili saba* Maili saba ni kama kilomita 11.2. kutoka Yerusalemu. 14 Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia. 15 Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akaja akatembea pamoja nao, 16 lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue.
17 Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?”
Wakasimama, nyuso zao zikionyesha huzuni. 18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamuuliza, “Je, wewe ndiye peke yako mgeni huku Yerusalemu ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?”
19 Akawauliza, “Mambo gani?”
Wakamjibu, “Mambo ya Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote. 20 Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulubisha. 21 Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye angelikomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatokee. 22 Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walikwenda kaburini leo alfajiri, 23 lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Yesu yu hai. 24 Kisha baadhi ya wenzetu walikwenda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona.”
25 Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii! 26 Je, haikumpasa Kristo† Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.kuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?” 27 Naye akianzia na Sheria ya Mose na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu yeye.
28 Nao walipokaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Yesu akawa kama anaendelea mbele. 29 Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, “Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia.” Basi akaingia ndani kukaa nao.
30 Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia. 31 Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena. 32 Wakaulizana wao kwa wao, “Je, mioyo yetu haikuwakawaka kwa furaha ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?”
33 Wakaondoka mara, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika 34 wakisema, “Ni kweli! Bwana amefufuka, naye amemtokea Simoni.” 35 Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Yesu alipoumega mkate.
Yesu Awatokea Wanafunzi Wake
(Mathayo 28:16-20; Marko 16:14-18; Yohana 20:19-23; Matendo 1:6-8)
36 Walipokuwa bado wanazungumza hayo, Yesu mwenyewe akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!”
37 Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka. 38 Lakini Yesu akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu? 39 Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi hasa. Niguseni mwone; kwa maana mzuka hauna nyama na mifupa, kama mnionavyo kuwa navyo.”
40 Aliposema haya, akawaonyesha mikono na miguu yake. 41 Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula chochote hapa?”
42 Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa, 43 naye akakichukua na kukila mbele yao.
44 Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Sheria ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”
45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. 46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. 48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
Kuahidiwa Kwa Roho Mtakatifu
49 “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo utokao juu.”
Kupaa Kwa Yesu Mbinguni
(Marko 16:19-20; Matendo 1:9-11)
50 Akiisha kuwaongoza mpaka kwenye viunga vya Bethania, akainua mikono yake juu na kuwabariki. 51 Alipokuwa anawabariki, akawaacha, akachukuliwa mbinguni. 52 Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. 53 Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu. Amen.