10
Mithali Za Solomoni
Mithali za Solomoni:
Mwana mwenye hekima
huleta furaha kwa baba yake,
lakini mwana mpumbavu
huleta huzuni kwa mama yake.
 
Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,
lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.
 
Bwana hawaachi waadilifu kukaa njaa,
lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.
 
Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini
lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.
 
Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi
ni mwana mwenye hekima,
lakini yeye alalaye wakati wa mavuno
ni mwana mwenye kuaibisha.
 
Baraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
 
Kumbukumbu ya mwenye haki itakuwa baraka,
lakini jina la mwovu litaoza.
 
Mwenye hekima moyoni hupokea maagizo,
lakini mpumbavu apayukaye huangamia.
 
Mtu mwadilifu hutembea salama,
lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagunduliwa.
 
10 Yeye akonyezaye kwa nia mbaya husababisha huzuni,
naye mpumbavu apayukaye huangamia.
 
11 Kinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
 
12 Chuki huchochea faraka,
lakini upendo husitiri mabaya yote.
 
13 Hekima hupatikana katika midomo ya wenye kupambanua,
lakini fimbo ni kwa ajili ya mgongo wake asiye na ufahamu.
 
14 Wenye hekima huhifadhi maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hualika maangamizi.
 
15 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,
bali ufukara ni maangamizi ya maskini.
 
16 Ujira wa wenye haki huwaletea uzima,
lakini mapato ya waovu huwaletea adhabu.
 
17 Anayekubali kuadibishwa yuko katika njia ya uzima,
lakini yeyote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.
 
18 Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo,
na yeyote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.
 
19 Wakati maneno ni mengi, dhambi haikosekani,
lakini yeye ambaye huzuia ulimi wake ni mwenye busara.
 
20 Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora,
bali moyo wa mwovu una thamani ndogo.
 
21 Midomo ya mwenye haki hulisha wengi,
lakini wapumbavu hufa kwa kukosa ufahamu.
 
22 Baraka ya Bwana hutajirisha,
wala haichanganyi huzuni.
 
23 Mpumbavu hufurahia tabia mbaya,
lakini mtu mwenye ufahamu hupendezwa na hekima.
 
24 Kile anachoogopa mwovu ndicho kitakachompata;
kile anachoonea shauku mwenye haki atapewa.
 
25 Tufani inapopita, waovu hutoweka,
lakini wenye haki husimama imara milele.
 
26 Kama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho,
ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.
 
27 Kumcha Bwana huongeza urefu wa maisha,
lakini miaka ya mwovu inafupishwa.
 
28 Tarajio la mwenye haki ni furaha,
bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.
 
29 Njia ya Bwana ni kimbilio kwa wenye haki,
lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.
 
30 Kamwe wenye haki hawataondolewa,
bali waovu hawatasalia katika nchi.
 
31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima,
bali ulimi wa upotovu utakatwa.
 
32 Midomo ya wenye haki inajua kile kinachofaa,
bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.