5
Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake! Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu. Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu. Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu, mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa Siku ile ya Bwana. Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga? Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa tambiko. Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli. Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi. 10 Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu ninyi kuihama dunia hii kabisa! 11 Nilichoandika ni hiki: msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye. 12 Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, ninyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu ninyi wenyewe? 13 Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu!