6
Baadaye, idadi ya wanafunzi ilipokuwa inazidi kuongezeka, kulitokea manung'uniko kati ya wanafunzi waliosema Kigiriki na wale waliosema Kiebrania. Wale waliosema Kigiriki walinung'unika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji wa mahitaji ya kila siku. Kwa hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema, “Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji wa mahitaji. Hivyo, ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo. Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri neno la Mungu.” Jambo hilo likaipendeza jumuiya yote ya waumini. Wakawachagua Stefano, mtu mwenye imani kubwa na mwenye kujawa na Roho Mtakatifu, Filipo, Prokoro, Nikanora, Timona, Parmena na Nikolao wa Antiokia ambaye hapo awali alikuwa ameongokea dini ya Kiyahudi. Wakawaweka mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono. Neno la Mungu likazidi kuenea na idadi ya waumini huko Yerusalemu ikaongezeka zaidi, na kundi kubwa la makuhani wakaipokea imani. Mungu alimjalia Stefano neema tele, akampa nguvu nyingi hata akawa anatenda miujiza na maajabu kati ya watu. Lakini watu fulani wakatokea ili wabishane na Stefano. Baadhi ya watu hao walikuwa wa sunagogi moja lililoitwa “Sunagogi la Watu Huru”, nao walitoka Kurene na Aleksandria; wengine walitoka Kilikia na Asia. 10 Lakini hawakuweza kumshinda kwa sababu ya hekima yake na kwa sababu ya yule Roho aliyeongoza maneno yake. 11 Kwa hiyo waliwahonga watu kadhaa waseme: “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kumkashifu Mose na kumkashifu Mungu.” 12 Kwa namna hiyo, waliwachochea watu, wazee na walimu wa Sheria. Basi, wakamjia Stefano, wakamkamata na kumleta mbele ya Baraza kuu. 13 Walileta Barazani mashahidi wa uongo ambao walisema, “Mtu huyu haachi kamwe kusema maneno ya kupakashifu mahali hapa patakatifu na Sheria ya Mose. 14 Kwa maana tulikwisha msikia akisema eti huyo Yesu wa Nazareti atapaharibu kabisa mahali hapa na kufutilia mbali desturi zile tulizopokea kutoka kwa Mose.” 15 Wote waliokuwa katika kile kikao cha Baraza walimkodolea macho Stefano, wakauona uso wake umekuwa kama wa malaika.