10
1 Nataka ninyi mjue kaka na dada zangu, ya kuwa baba zetu walikuwa chini ya wingu na wote walipita katika bahari. 2 Wote walibatizwa wawe wa Musa ndani ya wingu na ndani ya bahari, 3 na wote walikula chakula kile kile cha roho. 4 Wote walikunywa kinywaji kile kile cha roho. Maana walikunywa kutoka katika mwamba wa roho uliowafuata, na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. 5 Lakini Mungu hakupendezwa sana na wengi wao, na maiti zao zilisambazwa jangwani. 6 Basi mambo haya yote yalikuwa mifano kwetu, ili sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya kama na wao walivyofanya. 7 Msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa. Hii ni kama ilivyoandikwa, “Watu walikaa chini wakila na kunywa, na waliinuka kucheza kwa tamaa za mapenzi.” 8 Tusifanye uasherati kama wengi wao walivyofanya. Wakafa siku moja watu ishirini na tatu elfu kwa sababu hiyo. 9 Wala tusimjaribu Kristo, kama wengi wao walivyofanya na wakaharibiwa kwa nyoka. 10 Na pia msinung'unike, kama wengi wao walivyonung'unika na kuharibiwa na malaika wa mauti. 11 Basi mambo hayo yalitendeka kama mifano kwetu. Yakaandikwa ili kutuonya sisi - tuliofikiliwa na miisho ya zamani. 12 Kwa hiyo kila ajionaye amesimama awe makini asije akaanguka. 13 Hakuna jaribu lililowapata ninyi lisilo kawaida ya wanadamu. Ila Mungu ni mwaminifu. Hatawaacha mjaribiwe kupita uwezo wenu. Pamoja na jaribu yeye atawapa mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili. 14 Kwa hiyo, wapendwa wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. 15 Nasema nanyi kama watu wenye akili, ili muamue juu ya ninalosema. 16 Kikombe cha baraka tubarikicho, si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? 17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja. Sisi sote twapokea mkate mmoja kwa pamoja. 18 Watazameni watu wa Israeli: Je! Wale wote walao dhabihu si washiriki katika madhabahu? 19 Nasema nini basi? Ya kuwa sanamu ni kitu? Au ya kuwa chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? 20 Lakini nasema juu ya vitu vile wavitoavyo sadaka watu wapagani wa Mataifa, ya kuwa wanatoa vitu hivi kwa mapepo na sio kwa Mungu. Nami sitaki ninyi kushirikiana na mapepo! 21 Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mapepo. Hamwezi kuwa na ushirika katika meza ya Bwana na katika meza ya mapepo. 22 Au twamtia Bwana wivu? Tuna nguvu zaidi yake? 23 “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vifaavyo. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote viwajengavyo watu. 24 Hakuna hata mmoja angetafuta mazuri yake tu. Badala yake, kila mmoja angetafuta mazuri ya mwenzake. 25 Mnaweza kula kila kitu kiuzwacho sokoni bila kuuliza -uliza kwa ajili ya dhamiri. 26 Maana “dunia ni mali ya Bwana, na vyote viijazavyo.” 27 Na mtu asiyeamini akiwaalika kula, na mnataka kwenda, kuleni chochote awapacho pasipo kuuliza maswali ya dhamiri. 28 Lakini mtu akiwaambia, “Chakula hiki kimetokana na sadaka ya wapagani,” msile. Hii ni kwa ajili yake aliyewaambia, na kwa ajili ya dhamiri. 29 Nami simaanishi dhamiri zenu, bali dhamiri ya yule mwingine. Maana kwanini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine? 30 Ikiwa mimi natumia chakula kwa shukrani, kwanini nitukanwe kwa kitu ambacho nimeshukuru kwacho? 31 Kwa hiyo, chochote mnachokula au kunywa, au chochote mfanyacho, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu. 32 Msiwakoseshe Wayahudi au Wayunani, au kanisa la Mungu. 33 Jaribuni kama mimi ninavyojaribu kuwapendeza watu wote kwa mambo yote. Sitafuti faida yangu mwenyewe, bali ya wengi. Nami nafanya hivi ili wapate kuokolewa.