14
1 Wakati huo Abiya mwana wa Yeroboamu akawa mgonjwa sana. 2 Yeroboamu akamwambia mke wake, “amka ujibadilishe, ili wasikutambue kuwa wewe ndiye mke wangu, na uende Shilo, kwa sababu nabii Ahiya yuko huko, yeye ndiye aliyeninea mimi kuwa nitakuwa mfalme juu ya watu hawa. 3 Uchukue mikate kumi, na kaki na mtungi wa asali, na uende kwa Ahiya. Naye atakuambia kitakachotokea kwa mtoto.” 4 Mke wa Yeroboamu akafanya hivyo; akaenda Shilo mpaka kwenye nyumba ya Ahiya. Wakati huo Ahiya alikuwa hawezi kuona, kwa kuwa macho yake yalikuwa yameishiwa nguvu kwa sababu ya umri wake. 5 BWANA akamwambia Ahiya, “Tazama mke wa Ahiya anakuja kutafuta kutaka ushauri toka kwako kuhusiana na mwanae, kwa kuwa ni mgonjwa. Mwambie hivi na hivi, kwa sababu atakapofika atajifanya kuwa ni mwanamke mwingine.” 6 Naye Ahiya aliposikia sauti za miguu yake alipokuwa akiukaribia mlango, akasema, “karibu, mke wa Yeroboamu. Kwa nini unajifanya kuwa mtu mwingine? Nimetumwa kwako nikiwa na habaari mbaya. 7 Nenda ukamwambia Yeroboamu kwamba BWANA, Mungu wa Israeli, anasema, 'Nilikuinua kutoka kati ya watu na kukufanya uwe kiongozi wa watu wangu Israeli. 8 Niliugawa ufalme kutoka kwa Daudi na kukupa wewe, lakini bado hutaki kuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye alizishika amri zangu na kunifuata kwa moyo wake wote, na kufanya kilichokuwa sawa mbele ya macho yangu. 9 Badala yake, umefanya maovu, zaidi ya wote waliokutangulia. Umetengeneza miungu mingine, na umetengeneza sanamu za kuyeyushwa ili kunikasirisha na kunitupa nyuma yako. 10 Kwa hiyo, tazama, Nitaleta majanga kwenye familia yako; Nitawatupilia mbali watoto wako wote wa kiume katika Israeli, kama ni mtumwa au ni huru, na nitaiondoa familia yako, kama mtu anayechoma mavi mpaka yaishe. 11 Yeyote ambaye ni mwanafamilia yako atakayefia mjini ataliwa na mbwa, na yeyote atakayefia shamabani ataliwa na ndege wa angani, kwa kuwa Mimi BWANA, nimesema; 12 Kwa hiyo inuka wewe mke wa Yeroboamu, na uende nyumbani kwako; na mguu wako utakapokanyaga mjini, yule mtoto wa Abiya atakufa. 13 Na Israeli yote itamwombolezea na kumzika. Ni yeye pekee katika familia ya Abiya atakayepelekwa makaburini, kwa sababu ni yeye pekee yake kutoka kwenye nyumba ya Abiya, ambaye BWANA, Mungu wa Israeli alimwona kuwa ni mwema. 14 Pia BWANA atainua mfalme katika Israeli ambaye ataifutilia mbali familia ya Yeroboamu katika siku hiyo. Leo ndiyo siku hiyo, sasa hivi. 15 Kwa kuwa BWANA ataishambulia Israeli kama vile majani yanavyotikiswa majini, na ataing'oa Israeli katika nchi hii njema ambayo aliwpa mababu. Atawatawanya hata ng'ambo ya Mto Frati, kwa sababu wamefanya nguzo za Ashera kumkasirisha BWANA. 16 Ataiacha Israeli kwa sababu ya dhambi ya Yeroboamu, dhambi ambazo ametenda, na kwa hizo ameifanya Israeli kufanya dhambi. 17 Kwa hiyo mke wa Yeroboamu akainuka na akaondoka na akaenda mpaka Tirza. Naye alipofika kizingitini kwa nyumba yake, yule mtoto akafa. 18 Isareli wote wakamzika na kumwombolezea, kama vile alivyokuwa ameambiwa kwa neno la BWANA ambalo amelisema kupitia mtumishi wake nabii Ahiya. 19 Na kwa mambo mengine yanayOmhusu Yeroboamu, jinsi alivyopigana vita na jinsi alivyotawala, tazama yameandikwa katika kitabu cha matukio ya wafalme wa Israeli. 20 Yeroboamu alitawala kwa miaka ishirini na mbili naye akalala na babu zake, na Nadabu mwanawe akawa mfalme mahali pake. 21 Sasa Rehoboamu mwana wa Sulemani alikuwa mtawala wa Yuda. Rehoboamu alikuwa na umri wa miaka arobaini na moja alipokuwa mfalme, na akatawala kwa miaka kumi na saba kule Yerusalemu, mji ambao BWANA alikuwa ameuchagua kati ya makabila yote ya Israeli ili aweke jina lake kule. Jina la mama yake alikuwa Naama Mwamori. 22 Yuda ikafanya yaliyo maovu mbele ya macho ya BWANA; wakamtia wivu kwa makosa yao, zaidi ya yote ambayo baba zao walikuwa wamefanya 23 Kwa kuwa walijijengea wenyewe mahali pa juu, nguzo za mawe, na nguzo za Ashera katika kila mahali pa juu na katika kila mti wenye majani mabichi. 24 Pia kulikuwepo na ukahaba wa kipagani katika nchi. Walifanya machukizo yaleyale kama wa mataifa yale ambayo BWANA alikuwa amewafukuza kutoka kwa watu wa Israeli. 25 Ilitokea wakati wa mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu wakati Shishaki akiwa mfalme wa Misri, akaja kinyume na Yerusalemu. 26 Akaichukua hazina iliyokuwa kwenye nyumba ya BWANA, na ile hazina iliyokuwa kwenye nyumba ya Mfalme. Akachukua kila kitu; Pia alizichukua zile ngao za dhahabu ambazo Sulemani alikuwa ametengeneza. 27 Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba mahali pake na akazikabidhi kwa wakuu wa walinzi, ambao walilinda malango ya kuingia kwa mfalme. 28 Na ikawa kila mfalme alipoingia kwenye nyumba ya BWANA, wale walinzi walizibeba na baadaye walizirudisha katika chumba cha walinzi. 29 Lakini katika mambo mengine kuhusiana na Rehoboamu, na yote yale aliyofanya, je, hayakuandikwa kwenye kitabu cha matukio ya wafalme wa Yuda? 30 Kulikuwa na mapigano yasiyokoma kati ya nyumba ya Rehoboamu na nyumba ya Yeroboamu. 31 Kwa hiyo Rehoboamu akalala na mababu zake naye akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi Jina la mama yake alikuwa Naama Mwamori. Abiya mwanawe akawa mfalme mahali pake