5
1 Sammweli 5: 1-3 Basi Wafilisti wakawa wamelitwaa sanduku la Mungu, wakalileta kutoka Ebenezeri hadi Ashdodi. Wafilisti walilichukua sanduku la Mungu, wakalileta ndani ya nyumba ya Dagoni, na wakalikalisha pembeni mwa Dagoni. Watu wa Ashdodi walipoamka mapema siku ya pili, tazama, Dagoni ilianguka chini kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA. Hivyo waliichukua Dagoni na kuisimamisha tena katika sehemu yake.. Lakini walipoamka mapema kesho yake, tazama, Dagoni alikuwa ameanguka chini kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA. Kichwa cha Dagoni na vitanga vyake miwili vilikatika na kulala mlangoni. Kiwiliwili cha Dagoni ndicho kilibaki tu. Na hii ndiyo sababu, makuhani wa Dagoni na yeyote aingiae ndani ya nyumba ya Dagoni, hata leo, hawezi kukanyaga mlango wa Dagoni katika Ashdodi. Mkono wa BWANA ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi. Aliwaangamiza akawatesa kwa majipu, Ashdodi na wilaya zake kwa pamoja. Watu wa Ashdodi walipotambua kilichokuwa kinatokea, walisema, “Sanduku la Mungu wa Israeli lisikae kwetu, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya mungu wetu Dagoni.” Basi wakawatuma watu wawakusanye pamoja viongozi wote wa Wafilisti; wakawambia, “Tufanye nini na sanduku la Mungu wa Israeli?” Wakawajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli lihamishwe na kupelekwa Gathi.” Basi wakalihamisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli hadi huko Gathi. Lakini baada ya kulipeleka huko, mkono wa BWANA ulikuwa juu ya mji huo, ukasababisha machafuko makubwa. Akawatesa watu wa mji huo, wakubwa kwa wadogo; na majipu yakaota juu ya miili yao. 10 Basi, wakalipeleka sanduku la Mungu hadi Ekroni. Lakini mara tu sanduku la Mungu lilipoingia Ekroni, watu wa Ekroni walipiga kelele wakisema, “Wametuletea sanduku la Mungu wa Israeli kutuua sisi na watu wetu.” 11 Basi wakawatuma watu wawakusanye pamoja viongozi wote wa Wafilisti; wakawambia, “Lipelekeni mbali sanduku la Mungu wa Israeli, na lirudishwe katika makao yake, ili lisije kutuua sisi na watu wetu.” Kwa maana kulikuwa na hofu ya kutisha mjini mwote; Mkono wa Mungu ulikuwa mzito mno huko. 12 Watu ambao hawakufa waliteswa na majipu, na kilio cha mji kilipanda hadi mbinguni.