9
Samweli 9: 1-2 1 Basi kulikuwa na mtu mmoja kutoka Benyamini, mtu mashuhuri. Jina lake aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Zerori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini. 2 Huyu alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Sauli, kijana mzuri wa uso. Hapakuwapo mwanaume mzuri wa uso kuliko huyu miongoni mwa watu wote wa Israeli. Kutoka mabegani kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wengine. 3 Na punda wa Kishi, baba yake na Sauli walipotea. hivyo Kishi akamwambia Sauli mwanawe, “Mchukue mmoja wa watumishi; uamke uende kuwatafuta punda,” 4 Sauli akapita katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu na akaenda akapita katika nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona. Kisha walipita katika nchi ya Shaalimu, lakini hawakuwa huko. Baadaye alipita katika nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwaona wale punda. 5 Na walipofika nchi ya Sufu, Sauli alimwambia mtumishi wake aliyekuwa naye, “Njoo na turudi, pengine baba aweza kuacha kuchunga punda na kuanza kutuhofia sisi.” 6 Lakini mtumishi akamwmbia, “Sikiliza, Yupo mtu wa Mungu katika mji huu. Naye ni mtu wa kuheshimiwa sana; kila asemalo huwa kweli. Hebu twende huko; labda anaweza kutuambia tupitie wapi katika safari yetu.” 7 Ndipo Sauli akamwambia mtumish iwake, “Lakini kama tukienda kwake, twaweza kumpelekea nini? Maana hata mkate katika mfuko wetu umekwisha, na hakuna zawadi ya kumpelekea mtumishi wa Mungu. Tuna kitu gani? 8 Huyo mtumishi akamjibu Sauli na kusema, “Hapa, ninayo robo ya shekeli ya fedha ambayo nitampa mtumishi wa Mungu, atuambie ni njia ipi yatupasa tuiendee.” 9 (Zamani katika Israeli, mtu alipotaka kujua neno kuhusu mapenzi ya Mungu, alisema, “Njoo, haya twende kwa mwonaji.” Kwa maana nabii wa leo, zamani aliitwa Mwonaji). 10 Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, “Umesema vyema. Haya, njoo twende.” Basi wakaenda katika mji ambao mtu wa Mungu alikuwamo. 11 Walipopanda mlima kuelekea mjini, walikutana na wasichana wakienda kuteka maji; Sauli na mtumishi wake wakawauliza, “Mwonaji hupo hapa?” 12 Nao wakawajibu, na kusema, “Yupo; tazameni, yuko mbele yenu. Harakisheni, kwa maana anakuja mjini leo, sababu leo watu wanatoa dhabihu zao mahali pa juu. 13 Mara tu mtakapoingia mjini mtamuona, kabla hajapanda mahali pa juu kla chakula. Watu hawatakula hata atakapokuja, kwa sababu ndiye ataibariki dhabihu; na baadaye wale ambao wamealikwa hula. Basi pandeni, mtamuona sasa hivi.” 14 Kwa hiyo walikwea kwenda mjini. Walipokuwa wakiingia mjini, walimuona Samweli akija mbele yao, akipanda kwenda mahali pa juu. 15 Siku moja kabla Sauli hajafika, BWANA alikuwa amemfunulia Samweli: 16 “Kesho wakati kama huu nitakutumia mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe utamtia mafuta awe mfalme juu ya watu wangu Israeli. Atawaokoa watu wangu kutoka mkono wa Wafilisti. Kwa kuwa nimewaonea huruma watu wangu na kilio cha kutaka msaada kimenifikia.” 17 Samweli alipomuona Sauli, BWANA akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekwambia habari zake! Yeye ndiye atakayewatawala watu wangu.” 18 Ndipo Sauli akaja karibu na Samweli katika lango na kusema, “Niambie nyumba ya Mwonaji iko wapi? 19 Samweli akamjibu Sauli akisema, “Mimi ndiye mwonaji. Tangulia mbele hadi mahali pa juu, nami nitakueleza kila kitu kilichomoyoni mwako. 20 Kama punda wenu waliopotea siku tatu zilizopita, msihofu kuhusu hao punda, kwa kuwa wamekwishapatikana. Na yote yaliyotamanika kwa ajili ya Israeli yanamwangukia nani? Siyo kwako na nyumba ya baba yako yote?” 21 Sauli akamjibu na kusema, Siyo mimi Mbenyamini, kutoka kabila lililo dogo sana kwa makabila ya Israeli? Siyo ukoo wangu ulio mdogo sana kwa kabila la Benyamini? Kwa nini basi unaniambia kwa namna hii?” 22 Hivyo Samweli akamchukua Sauli na mtumishi wake, akawaingiza ukumbini, akawakalisha mahali pa heshima pa wale walioalikwa, idadi yao takribani watu thelathini. 23 Samweli akamwambia mpishi, “Lete sehemu niliyokupatia, sehemu ambayo nilikwambia hivi, “Itenge.”' 24 Basi mpishi alichukua paja lililokuwa limeinuliwa katika dhabihu na kile kilichokuwa pamoja nalo, akaitenga mbele ya Sauli. Kisha Samweli akasema, “Angalia kile kilichokuwa kimetunzwa kwa ajili yako! Kula, kwa sababu kilitunzwa hadi wakati maalum ufike kwa ajili yako. Na kwa sasa waweza kusema, 'Nimewaalika watu.”' Kwa hiyo Sauli alikula pamoja na Samweli siku hiyo. 25 Walipokuwa wamekwisha shuka chini kutoka sehemu ya juu na kuingia mjini, Samweli akazungumza na Sauli darini. 26 Na kulipopambazuka, Samweli alimwita Sauli darini na kusema, “Amka, kusudi nikusindikize uende zako,” Hivyo Sauli aliamka, na wote wawili, yeye na Samweli walitoka kwenda mtaani. 27 Walipokuwa wakienda nje ya viunga vya mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi wako atanguliye mbele yetu(na alitangulia mbele), Lakini wewe sharti usubiri kidogo, nipate kukuambia ujumbe wa Mungu.”