13
1 Ikawa baada ya hayo kwamba Amnoni mwana wa Daudi, akamtamani sana Tamari dada yake wa kambo aliyekuwa mzuri, alikuwa tumbo moja na Absalome, mwana wingine wa Daudi. 2 Amnoni akasononeka sana kiasi cha kuugua kwa ajili ya Tamari dada yake. Tamari alikuwa bikra, na hivyo ilionekana haiwezekani Amnoni kufanya neno lolote kwake. 3 Lakini Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yehonadabu mwana wa Shama, nduguye Daudi. 4 Yehonadabu alikuwa mtu mwelevu sana. Akamwambia Amnoni, “Kwa nini, mwana wa mfalme, unadhoofika kila siku? Kwa nini uniambii? Ndipo Amnoni akamjibu, “Nampenda Tamari, dada yake Absalome ndugu yangu.” 5 Ndipo Yehonadabu akamwambia, “Lala kitandani mwako na ujifanye kuwa mgonjwa. Wakati baba yako atakapo kuja kukuona, mwambie, Tafadhari mtume dada yangu Tamari aandaye chakula mbele yangu, ili kwamba nikione na kula kutoka mkononi mwake?” 6 Hivyo Amnoni akalala na kujifanya kuwa mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia mfalme, “Tafadhari mtume Tamari dada yangu aandaye chakula kwa ajili ya ugonjwa wangu mbele yangu ili kwamba nikile kutoka mkononi mwake. 7 Ndipo Daudi katika kasri lake akatuma neno kwa Tamari, kusema, “Nenda katika nyumba ya nduguyo Amnoni na umwandalie chakula. Hivyo 8 Tamari akaenda katika nyumba ya Amnoni nduguye alipokuwa amelala. Akachukua donge na kulifinyanga na kuandaa mkate mbele zake, kisha akauoka. 9 Akachukua kikaangio na kumpa mkate, lakini akakataa kula. Kisha Amnoni akawambia waliokuwepo, “Kila mtu na aondoke.” Hivyo kila mmoja akaondoka. 10 Amnoni akamwambia Tamari, “Lete chakula chumbani kwangu nikile katika mkono wako.” Tamari akachukua mkate aliokuwa ameuandaa, na kuuleta katika chumba cha Amnoni kaka yake. 11 Alipoleta chakula kwake, Amnoni akamshikilia na kumwambia, “Njoo, ulale nami, dada yangu.” 12 Yeye akamjibu, “Hapana, kaka yangu, usinilazimishe, kwani hakuna jambo kama hili linapaswa kufanyika katika Israeli. Usifanye jambo la aibu kiasi hiki! 13 Nitakwenda wapi ili nijiepushe na aibu ambayo jambo hili litaileta juu ya maisha yangu? Na tendo hili litakuonesha kuwa mpumbavu usiye na aibu katika Israeli yote. Tafadhari, ninakuomba uongee na mfalme. Yeye atakuruhusu unioe.” 14 Lakini Amnoni hakuweza kumsikiliza. Kwa kuwa alikuwa zaidi akamkamata na akalala naye. 15 Kisha Amnoni akamchukia Tamari kwa chuki kuu. Akamchukia zaidi ya jinsi alivyokuwa amemtamani. Amnoni akamwambia, “Inuka na uondoke.” 16 Lakini yeye akamjibu, “Hapana! kwa maana uovu wa kunifanya ni uondoke ni mbaya zaidi ya kile ulichonitenda!” Lakini Amnoni hakumsikiliza. 17 Badala yake, akamwita mtumishi wake na akasema, “Mwondoe mwanamke huyu mbele yangu, na uufunge mlango nyuma yake.” 18 Hivyo mtumishi wake akamtoa na kufunga mlango. Tamari alikuwa amevaa vazi lilinakishiwa kwani ndivyo binti za wafalme waliobikra valivyokuwa wakivaa. 19 Tamari akaweka majivu juu ya kichwa chake na akalirarua vazi lake 20 Absalome, kaka yake, akamwambia, “Amnoni, kaka yako, amekuwa nawe? Lakini sasa nyamaza, dada yangu. Yeye ni kaka yako. Usiliweke hili moyoni.” Hivyo Tamari akakaa peke yake katika nyumba ya Absalomu kaka yake. 21 Mfalme Daudi aliposikia haya yote, alikasirika sana. 22 Absalome hakusema chochote kwa Amnoni, kwa maana Absalome alimchukia kwa kile alichokifanya, kumdhalilisha Tamari, dada yake. 23 Ikawa baada ya miaka miwili mizima Absalomu akawa na wakatao kondoo manyoya wakifanya kazi huko Baali Hazori, ulioko karibu na Efraim, naye Absalomu akawaarika wana wote wa mfalme kufika huko. 24 Absalomu akamwendea mfalme na kusema, “Tazama sasa, mtumishi wako anao wakatao kondoo manyoya. Tafadhari, naomba mfalme na watumishi wake waende nami, mtumishi wako.” 25 Mfalme akamjibu Absalomu, “hapana mwanangu, tusiende sisi yote kwani tutakuwa mzigo kwako.” Absalomu akamhakikishia mfalme, lakini yeye asikubali kwenda, ila alimbariki Absalomu. 26 Kisha Absalomu akasema, “kama sivyo, basi tafadhari mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi.” Mfalme akamuliza, “Kwa nini Amnoni aende nanyi?” 27 Absalomu akamsihi Daudi, hivyo akamruhusu Amnoni na wana wengine wa mfalme kwenda naye. 28 Absalomu akawaamuru watumishi wake kusema, “Sikilizeni kwa makini. Amnoni atakapokuwa amelewa mvinyo, na nitakapowambia, 'Mpigeni Amnoni,' msiogope mwueni. Je siyo mimi niliyewamru? Mwe jasiri na hodari.” 29 Hivyo watumishi wa Absalome wakamtendea Amnoni kama walivyoamriwa. Kisha wana wote wa mfalme wakainuka na kila mmoja akapanda nyumbu wake akakimbia. 30 Hata ikawa wakati wakiwa njiani habari zikafika kwa Daudi kusema, “Absalomu ameua wana wote wa mfalme na hakuna hata mmoja aliyesalia.” 31 Kisha mfalme akainuka na kurarua mavazi yake na kujilaza juu ya sakafu; watumishi wake wote wakasimama karibu naye mavazi yao yameraruriwa. 32 Yehonadabu mwana wa Shama, nduguye Daudi, akajibu na kusema, “Bwana wangu asidhani kuwa vijana wote ambao ni wana wa mfalme wameuawa, kwa maana ni Amnoni pekee ndiye aliyeuawa. Absalomu alilipanga jambo hili tangu siku ile Amnoni alivyomwaribu Tamari, dada yake. 33 Kwa hiyo basi, bwana wangu mfalme asiiweke taarifa hii moyoni, kudhani kwamba wana wote wa mfalme wameuawa, kwani aliyeuawa ni Amnoni peke yake.” 34 Absalomu akakimbia. Mtumishi aliyekuwa akiangalia akainua macho yake na kuona watu wengi wakija njiani kando ya kilima upande wake wa magharibi. 35 Kisha Yehonadabu akamwambia mfalme, “Tazama, wana wa mfalme wanakuja. kama mtumishi wako alivyosema.” 36 Ikawa mara alipomaliza kusema wana wa mfalme wakafika, wakainua sauti zao na kulia. Na mfalme pamoja na watumishi wake wote pia wakalia kwa uchungu. 37 Lakini Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Mfalme akaomboleza kila siku kwa ajili ya mwanaye. 38 Hivyo Absalomu akakimbia na kwenda Geshuri na akakaa huko kwa miaka mitatu. 39 Moyo wa mfalme Daudi ukatamani kwenda kumwona Absalomu, kwa maana alikuwa amefarijika kwa habari ya kifo cha Amnoni.