6
1 Sasa katika siku hizi, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa inaongezeka, lalamiko la Wayahudi wa Kiyunani lilianza dhidi ya Waebrania, kwa sababu wajane wao walikuwa wanasahaulika katika mgao wa kila siku wa chakula. 2 Mitume kumi na wawili waliwaita kusanyiko lote la wanafunzi na kusema, “Siyo sahihi kwetu kuliacha neno la Mungu na kuhudumia mezani. 3 Kwa hiyo, ndugu, chagueni, wanaume saba, kutoka miongoni mwenu, watu wema, waliojaa Roho na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi huduma hii. 4 Na sisi, tutaendelea daima katika kuomba na katika huduma ya neno.” 5 Hotuba yao ikaupendeza mkutano wote. Hivyo, wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena, na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia. 6 Waumini waliwaleta watu hawa mbele ya mitume, walioomba na badaye wakawawekea mikono yao. 7 Hivyo, neno la Mungu lilienea; na idadi ya wanafunzi ilizidi kuongezeka huko Yesrusalem; na idadi kubwa ya makuhani wakaitii imani. 8 Na Stefano, aliyejaa neema na nguvu, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa miongoni mwa watu. 9 Lakini hapo wakainuka baadhi ya watu wafuasi wa Sinagogi liitwalo Sinagogi la Mahuru, na la Wakirene na la Waeskanderia, na baadhi kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa walikuwa wakihojiana na Stefano. 10 Lakini, hawakuweza kushindana na hekima na Roho ambayo Stefano alikuwa akitumia katika kuzungumza. 11 Kisha waliwashawishi baadhi ya watu kwa siri kusema, “Tumesikia Stefano akizungumza maneno ya kufuru dhidi ya Musa na dhidi ya Mungu.” 12 Waliwashurutisha watu, wazee, na waandishi, na kumwendea Stefano, wakamkamata, na kumleta mbele ya baraza. 13 waliwaleta mashahidi wa uongo, waliosema, “mtu huyu haachi kunena maneno mabaya dhidi ya eneo hili takatifu na sheria. 14 Kwani tumemsikia akisema kwamba huyu Yesu wa Nazareti atapaharibu mahali hapa na kuzibadili desturi tulizokabidhiwa na Musa.” 15 Kila mmoja aliyekuwa katika baraza, akaelekeza macho yake kumwangalia Stefano, nao wakauona uso wake ulikuwa kama uso wa malaika.