23
1 Paulo akawaangalia moja kwa moja watu wa baraza na kusema, “Ndugu zangu, nimeishi mbele za Mungu kwa dhamira nzuri hadi hivi leo.” 2 Kuhani mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. 3 Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Umekaa ukinihukumu kwa sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?” 4 Wale waliokuwa wamesimama karibu naye wakasema, “Hivi ndivyo unavyomtukana kuhani mkuu wa Mungu?” 5 Paulo akasema, “ndugu zangu, mimi sikujua kwamba huyu ni kuhani mkuu. Kwa kuwa imeandikwa, hutazungumza vibaya juu ya mtawala wa watu wako.” 6 Paulo alipoona ya kwamba upande mmoja wa baraza ni Masadukayo na wengine Mafarisayo, akapaza sauti na kusema, “ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Ni kwa sababu hii nategemea kwa ujasiri ufufuo wa wafu ninao hukumiwa nao.” 7 Alipoyasema haya, malumbano makubwa yakatokea baina ya Mafarisayo na Masadukayo, na mkutano ukagawanyika. 8 Kwani Masadukayo husema hakuna ufufuo, malaika wala hakuna roho, ila Mafarisayo husema haya yote yapo. 9 Ghasia kubwa ikatokea na baadhi ya waandishi waliokuwa upande wa Mafarisayo wakasimama na kujadili, wakisema, “hatujaona chochote kibaya dhidi ya mtu huyu. Vipi kama roho au malaika ameongea na yeye?” 10 Wakati kulitokea hoja kubwa, mkuu wa majeshi aliogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipande vipande na wao, hivyo akaamuru wanajeshi washuke chini na kumchukua kwa nguvu kutoka kwa wajumbe wa baraza, na kumleta katika ngome. 11 Usiku uliofuata Bwana alisimama karibu naye na kusema, “Usiogope, kwa kuwa umenishuhudia katika Yerusalemu, hivyo utatoa ushahidi pia katika Roma.” 12 Kulipokucha, baadhi ya Wayahudi walifanya agano na kuita laana juu yao wenyewe: walisema ya kwamba hawatakula wala kunywa chochote mpaka watakapomuua Paulo. 13 Kulikuwa na watu zaidi ya arobaini ambao walifanya njama hii. 14 wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejiweka wenyewe kwenye laana kuu, tusile chochote hadi tutakapomwua Paulo. 15 Hivyo sasa, baraza limwambie jemadari mkuu amlete kwenu, kana kwamba mnaamua kesi yake kwa usahihi. Kwetu sisi tuko tayari kumwua kabla hajaja hapa.” 16 Lakini mtoto wa dada yake na Paulo akasikia kwamba kulikuwa na njama, akaenda akaingia ndani ya ngome na kumwambia Paulo. 17 Paulo akamwita akida mmoja akasema, “Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwambia.” 18 Basi akida akamchukua yule kijana akampeleka kwa jemedari mkuu akamwambia, “Paulo yule mfungwa aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwako. Ana neno la kukuambia.” 19 Yule jemadari mkuu akamshika kwa mkono akajitenga naye kando, na akamwuliza, “Ni kitu gani unachotaka kuniambia?” 20 Kijana yule akasema, “Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo kesho kwenye baraza kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahili zaidi. 21 Basi wewe usikubali kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamvizia. Wamejifunga kwa laana, wasile wala wasinywe hata watakapomwua. Hata sasa wako tayari, wakisubiria kibali toka kwako.” 22 Basi yule jemadari mkuu akamwacha kijana aende zake, baada ya kumwagiza “usimwambie mtu yeyote ya kwamba umeniarifu haya.” 23 Akawaita maakida wawili akasema watayarisheni askari mia mbili kwenda Kaisaria na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, mtaondoka zamu ya tatu ya usiku. 24 Akawaambia kuweka wanyama tayari ambaye Paulo atamtumia na kumchukua salama kwa Feliki Gavana. 25 Akaandika barua kwa namna hii, 26 Klaudio Lisia kwa Liwali mtukufu Feliki, salamu. 27 Mtu huyu alikamatwa na wayahudi wakawa karibu kumwua, ndipo nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata habari ya kuwa yeye ni raia wa kirumi. 28 Nilitaka kujua kwa nini wamemshtaki, hivyo nikampeleka kwenye baraza. 29 Nikaona kwamba alikuwa ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sheria yao, wala hakushitakiwa neno lolote la kustahili kuuawa wala kufungwa. 30 Kisha ikajulikana kwangu kwamba kuna njama dhidi yake, hivyo kwa haraka nikamtuma kwako, na kuwaagiza wanaomshitaki pia walete mashitaka dhidi yake mbele yako. Wakaagana.” 31 Basi wale askari wakatii amri: wakamchukua Paulo wakampeleka hata Antipatri usiku. 32 Siku iliyofuata, maaskari wengi wakawaacha wale wapanda farasi waende pamoja naye, nao wakarudi zao ngomeni. 33 Na wapanda farasi walipofika Kaisaria, na kumpa liwali ile barua, wakamweka Paulo mbele yake. 34 Naye liwali alipoisoma barua, alimuuliza Paulo alitokea jimbo gani; alipojua ya kwamba ni mtu wa Kilikia, 35 akasema, “Nitakusikia wewe watakapo kuja wale waliokushitaki,” akaamuru awekwe katika ikulu ya Herode.