27
1 Ilipoamuliwa kwamba tunatakiwa tusafiri kwa maji kwenda Italia, walimkabidhi Paulo na wafungwa wengine kwa afisa mmoja wa jeshi la Kiroma aliyeitwa Julio, wa Kikosi cha Agustani. 2 Tukapanda meli kutoka Adramitamu, ambayo ilikuwa isafiri kandokando ya pwani ya Asia. Hivyo tukaingia baharini. Aristaka kutoka Thesolanike ya Makedonia akaenda pamoja nasi. 3 Siku iliyofuata tukatua nanga katika mji wa Sidoni, ambapo Julio alimtendea Paulo kwa ukarimu na akamruhusu kwenda kwa rafiki zake kupokea ukarimu wao. 4 Kutoka hapo tukaenda baharini tukasafiri kuzunguka kisiwa cha Kipro ambacho kilikuwa kimeukinga upepo, kwa sababu upepo ulikuwa ukitukabili. 5 Baada ya kuwa tumesafiri katika maji yaliyo karibu na Kilikia na Pamfilia, tukaja Mira, mji wa Lisia. 6 Pale yule afisa wa jeshi la Kiroma, akaikuta meli kutoka Alexandria ambayo ilikuwa isafiri kuelekea Italia. Akatupandisha ndani yake. 7 Baada ya kuwa tumesafiri polepole kwa siku nyingi na hatimaye tukawa tumefika kwa taabu karibu na Kinidas, upepo haukuturuhusu tena kuelekea njia hiyo, hivyo tukasafiri kandokando ya kivuli cha Krete tukiukinga upepo, mkabala na Salmone. 8 Tukasafiri kandokando ya pwani kwa ugumu, mpaka tukafika mahali palipoitwa Fari Haveni ambayo iko karibu na mji wa Lasi. 9 Tulikuwa tumechukua muda mwingi sana, na muda wa mfungo wa Kiyahudi ulikuwa umepita pia, na sasa ilikuwa ni hatari kuendelea kusafiri. Hivyo Paulo akatuonya, 10 na kusema, “Wanaume, naona safari ambayo tunataka tuichukue itakuwa na madhara na hasara nyingi, siyo tu ya mizigo na meli, lakini pia ya maisha yetu.” 11 Lakini afisa wa jeshi la Kiroma akamsikiliza zaidi bwana wake na mmiliki wa meli, kuliko mambo yale ambayo yalizungumzwa na Paulo. 12 Kwa sababu bandari haikuwa sehemu rahisi kukaa wakati wa baridi, mabaharia wengi wakashauri tusafiri kutoka pale, ili kwa namna yoyote tukiweza kuufikia mji wa Foinike, tukae pale wakati wa baridi. Foinike ni bandari huko Krete, na inatazama kaskazini mashariki na kusini mashariki. 13 Upepo wa kusini ulipoanza kuvuma polepole, mabaharia wakafikiri wamepata kile ambacho walikuwa wanakihitaji. Wakang'oa nanga na kusafiri kandokando ya Krete karibu na pwani. 14 Lakini baada ya muda mfupi upepo mkali, ulioitwa Wa kaskazini mashariki, ukaanza kutupiga kutoka ng'ambo ya kisiwa. 15 Wakati meli ilipolemewa na kushindwa kuukabili upepo, tukakubaliana na hali hiyo, tukasafirishwa nao. 16 Tukakimbia kupitia ule upande uliokuwa unaukinga upepo wa kisiwa kiitwacho Kauda; na kwa taabu sana tulifanikiwa kuuokoa mtumbwi. 17 Baada ya kuwa wameivuta, walitumia kamba kuifunga meli. Waliogopa kwamba tungeweza kwenda kwenye eneo la mchanga mwingi la Syiti, hivyo wakashusha nanga na waliendeshwa kandokando. 18 Tulipigwa kwa nguvu sana na dhoruba, hivyo siku iliyofuata mabaharia wakaanza kutupa mizigo kutoka melini. 19 Siku ya tatu, mabaharia wakaanza kuyatoa maji kwa mikono yao wenyewe. 20 Wakati ambapo jua na nyota hazikutuangazia kwa siku nyingi, bado dhoruba kubwa ilitupiga, na matumaini kwamba tungeokolewa yalitoweka. 21 Baada ya kuwa wameenda muda mrefu bila chakula, hapo Paulo akasimama katikati ya mabaharia akasema, “Wanaume, mlipaswa mnisikilize, na tusingengo'a nanga kutoka Krete, ili kupata haya madhara na hasara. 22 Na sasa nawafariji mjitie moyo, kwa sababu hakutakuwa upotevu maisha kati yenu, isipokuwa hasara ya meli tu. 23 Kwa sababu usiku uliopita malaika wa Mungu, ambaye huyo Mungu mimi ni wake, na ambaye ninamwabudu pia - malaika wake alisimama pembeni mwangu 24 na kusema, “Usiogope Paulo. Lazima usimame mbele ya Kaisari, na tazama, Mungu katika wema wake amekupa hawa wote ambao wanasafiri pamoja nawe. 25 Hivyo, wanaume, jipeni moyo, kwa sababu namwamini Mungu, kwamba itakuwa kama nilivyoambiwa. 26 Lakini lazima tuumie kwa kupigwa katika baadhi ya visiwa.” 27 Ulipofika usiku wa kumi na nne, tulipokuwa tukiendeshwa huko na huko kwenye bahari ya Adratik, kama usiku wa manane hivi, mabaharia walifikiri kwamba wamekaribia nchi kavu. 28 Walitumia milio kupima kina cha maji na wakapata mita thelathini na sita, baada ya muda mfupi wakapima tena wakapata mita ishirini na saba. 29 Waliogopa kwanza tunaweza kugonga miamba, hivyo wakashusha nanga nne kutoka katika sehemu ya kuwekea nanga na wakaomba kwamba asubuhi ingekuja mapema. 30 Wale mabaharia walikuwa wanatafuta namna ya kuitelekeza ile meli na walizishusha majini boti ndogo ndogo za kuokolea maisha, na wakajifanya kwamba wanatupa nanga kutoka sehemu ya mbele ya boti. 31 Lakini Paulo akamwambia yule askari wa jeshi la Kiroma na wale askari, “Hamuwezi kuokoka isipokuwa hawa watu wanabaki kwenye meli”. 32 Kisha wale askari wakakata kamba za ile boti na ikaachwa ichukuliwe na maji. 33 Wakati mwanga wa asubuhi ulipokuwa unajitokeza, Paulo akawasihi wote angalau wale kidogo. Akasema, “Hii ni siku ya kumi na nne mnasuburi bila kula, hamjala kitu. 34 Hivyo nawasihi mchukue chakula kidogo, kwa sababu hii ni kwa ajili ya kuishi kwenu; na hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea. 35 Alipokwisha kusema hayo, akachukua mkate akamshukuru Mungu mbele ya macho ya kila mtu. Kisha akaumega mkate akaanza kula. 36 Kisha wote wakatiwa moyo na wao wakachukua chakula. 37 Tulikuwa watu 276 ndani ya meli. 38 Walipokwisha kula vya kutosha, waliifanya meli nyepesi kwa kutupa ngano ndani ya bahari. 39 Ilipokuwa mchana, hawakuitambua nchi kavu, lakini wakaona sehemu ya nchi kavu iliyoingia majini iliyokuwa na mchanga mwingi. wakajadiliana kama wanaweza kuiendesha meli kuelekea hapo. 40 Hivyo wakazilegeza nanga wakaziacha baharini. Katika muda huo huo wakazilegeza kamba za tanga na wakaiinua sehemu ya mbele kuelekea kwenye upepo, hivyo wakaelekea kwenye hiyo sehemu ya mchanga mwingi. 41 Lakini wakaja mahali ambapo mikondo miwili ya maji inakutana, na meli ikaelekea mchangani. Na ile sehemu ya mbele ya meli ikakwama pale na haikuweza kutoka, lakini sehemu ya mbele ya meli ikaanza kuvunjika kwa sababu ya ukali wa mawimbi. 42 Mpango wa wale askari ulikuwa ni kuwaua wafungwa, ili kwamba hakuna ambaye angeogelea na kutoroka. 43 Lakini yule askari wa jeshi la Kiroma alitaka kumwokoa Paulo, hivyo akausimamisha mpango wao; na akawaamuru wale ambao wanaweza kuogelea, waruke kutoka melini kwanza na waende nchi kavu. 44 Kisha wanaume wengine watafuata, wengine juu ya vipande vya mbao na wengine juu ya vitu vingine kutoka kwenye meli. Kwa njia hii ikatokea kwamba wote tutafika salama nchi kavu.