26
1 Utakapofika katika nchi ambayo Yahwe Mungu wako anakupatia kama urithi, na utakapoimiliki na kuishi ndani yake, 2 basi unatakiwa kuchukua baadhi ya mavuno yote ya kwanza ya ardhi uliyoyaleta kutoka katika nchi ambayo Yahwe Mungu wako anakupatia. Unatakiwa kuyaweka ndani ya kikapu na kuelekea katika eneo ambalo Yahwe Mungu wako atapachagua kama mahali patakatifu. 3 Unatakiwa kwenda kwa kuhani ambaye atakuwa akihudumu katika siku hizo na kumwambia, “Siku ya leo ninakiri kwa Yahwe Mungu wako ya kuwa nimekuja katika nchi ambayo Yahwe aliapa kwa mababu zetu kutupatia”. 4 Kuhani anatakiwa kuchukua kikapu mkononi mwako na kukiweka madhabahuni ya Yahwe Mungu wako. 5 Unapaswa kusema mbele ya Yahwe Mungu wako, “Babu yangu alikuwa Mwaremi mzururaji. Alikwenda chini hadi Misri na kukaa kule, na idadi ya watu wake ilikuwa chache. Kule akawa taifa kubwa, lenye nguvu na idadi kubwa. 6 Wamisri walitutendea vibaya na kututesa. Walitulazimisha kufanya kazi za watumwa. 7 Tulimlilia Yahwe, Mungu wa baba zetu, naye akasikia sauti yetu na kuona mateso yetu, kazi zetu na mateso yetu. 8 Yahwe alituondoa Misri kwa mkono wake mkuu, kwa mkono wake ulionyoshwa, kwa hofu kuu, kwa ishara na miujiza; 9 na ametuleta katika sehemu hii na kutupatia nchi hii, nchi inayotiririka kwa maziwa na asali. 10 Tazama sasa, nimeleta mavuno ya kwanza kutoka katika nchi ambayo wewe, Yahwe, umenipatia. ” Unapaswa kuweka chini mbele ya Yahwe Mungu wako na kuabudu mbele zake; 11 na unapaswa kufurahia katika mema yote ambayo Yahwe Mungu wako amekufanyia, kwa ajili na nyumba yako – wewe, na Mlawi, na mgeni aliye miongoni mwako. 12 Utakapomaliza kutoa zaka yote ya mavuno katika mwaka wa tatu, yaani, mwaka wa kutoa zaka, basi unapaswa kuwapatia Mlawi, kwa mgeni, kwa yatima, na kwa mjane, ili kwamba waweze kula ndani ya malango yenu ya mji na kujazilishwa. 13 Unatakiwa kusema mbele ya Yahwe Mungu wako, “Nimetoa kutoka nyumbani mwangu vitu ambavyo ni mali ya Yahwe, na kumpatia Mlawi, mgeni, yatima, na mjane, kulingana na amri zote ulizonipatia. Sijavunja amri yako yoyote, wala sijazisahau. 14 Sijala kati yao wakati wa maombolezo yangu, wala sijaziweka mahali pengine nilipokuwa mchafu, wala sijazitoa kati yao kwa heshima ya wafu. Nimesikiliza sauti ya Yahwe Mungu wangu; Nimetii kila kitu ulichoniamuru kukifanya. 15 Tazama chini kutoka mahali patakatifu unapoishi, kutoka mbinguni, na ubariki watu wako Israeli, na nchi uliyotupatia, kama ulivyoapa kwa mababu zetu, nchi inayotiririka kwa maziwa na asali. 16 Leo Yahwe Mungu wako anawaamuru kuzitii sheria na amri hizi; basi utazishikilia na kuzitenda kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote. 17 Umetamka leo ya kuwa Yahwe ni Mungu wako, na kwamba utatembea katika njia zake na kushikilia sheria zake, maagizo yake na amri zake, na kwamba utaisikiliza sauti yake. 18 Leo Yahwe ametamka ya kwamba mu watu ambao ni mali yake, kama alivyoahidi kwenu, na kwamba mnapaswa kushikilia amri zake zote. 19 Na atawaweka juu zaidi ya mataifa mengine aliyoyaumba nanyi mtapokea sifa, umaarufu na heshima. Mtakuwa watu waliowekwa kando kwa Yahwe Mungu wako, kama alivyosema.”