2
1 Ndugu zangu msiifuate imani ya Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, kwa kupendelea watu fulani. 2 Kama mtu fulani akiingia kwenye mikutano yenu amevaa pete za dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia masikini mwenye mavazi machafu, 3 na mkaonyesha kumjali zaidi yule mwenye mavazi mazuri na kusema, “Tafadhari wewe keti hapa mahali pazuri” lakini mkamwambia yule masikini, “Wewe simama pale,” au “Kaa chini ya miguu yangu.” 4 Je, hamuhukumiani ninyi wenyewe, na kuwa waamuzi wenye mawazo mabaya? 5 Sikilizeni, ndugu zangu wapendwa, je, Mungu hakuwachagua masikini wa dunia kuwa matajiri katika imani na kurithi ufalme aliowaahidia wampendao? 6 Lakini mmewadharau masikini! Je, sio matajiri wanaowatesa ninyi, na sio wao wanaowaburuta mahakamani? 7 Je, si matajiri wanaolitukana jina lile zuri ambalo kwalo mnaitiwa? 8 Hata hivyo, kama mwaitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa katika maandiko, “Utampenda jirani yako kama wewe mwenyewe,” mwafanya vyema. 9 Lakini kama mkipendelea baadhi ya watu, mnatenda dhambi, mwahukumiwa na sheria kuwa ni wavunja sheria. 10 Kwa kuwa yeyote atiiye sheria yote, na bado akajikwaa katika nukta moja tu, amekuwa na hatia ya kuvunja sheria yote! 11 Kwa kuwa Mungu aliyesema, “Usizini,” ndiye pia aliyesema, “Usiue.” Kama hauzini, lakini una uwa, umekwishavunja sheria ya Mungu. 12 Kwa hiyo zungumzeni na kutii kama wale ambao mko karibu kuhukumiwa na sheria ya uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu huja pasipo huruma kwa wale wasio na huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu. 14 Kuna uzuri gani, ndugu zangu, kama mtu anasema ninayo imani, lakini hana matendo? Je, imani hiyo yaweza kumwokoa? 15 Kama ndugu wa kiume au wa kike ni muhitaji wa mavazi au chakula cha kila siku, 16 na mmoja wenu akawaambia, “Nendeni kwa amani, mkaote moto na mle vizuri,” lakini hamuwapi mahitaji muhimu ya mwili, hiyo yafaaa nini? 17 Hali kadhalika, imani pekee, kama haina matendo, imekufa. 18 Bado mtu fulani anaweza kusema, “ Una imani, na mimi ninayo matendo.” Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu. 19 Waamini kuwa kuna Mungu mmoja; uko sahihi. Lakini mapepo nayo yanaamini hivyo na kutetemeka. 20 Je, unataka kujua, ewe mtu mpumbavu, namna ambavyo imani hiyo pasipo matendo isivyofaa? 21 Je, si baba yetu Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo alipomtoa mwanawe Isaka juu ya madhabahu? 22 Mnaona kuwa imani yake ilifanya kazi na matendo yake, na kwa matendo yake, imani yake ilifikia kusudio lake. 23 Maandiko yalitimizwa yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu, na akahesabiwa kuwa ni mwenye haki.” Hivyo Abrahamu aliitwa rafiki wa Mungu. 24 Mwaona kuwa kwa matendo mtu huhesabiwa haki, na si kwa imani tu. 25 Hali kadhalika, je, hakuwa Rahabu yule kahaba alihesabiwa haki kwa matendo, alipowakaribisha wajumbe na kuwapeleka kwa barabara nyingine? 26 Kwa kuwa kama vile mwili usipokuwa na roho umekufa, vivyo hivyo imani pasipo matendo imekufa.