5
Njoni sasa, enyi mlio matajiri, lieni kwa sauti ya juu kwa sababu ya taabu inayokuja juu yenu. Utajiri wenu umeharibiwa na mavazi yenu yametafunwa na wadudu waharibifu. Dhahabu zenu na fedha zenu zimekosa thamani, na uharibifu wake utashuhudia dhidi yenu na kuangamiza miili yenu kama moto. Mmejiwekea hazina yenu katika siku za mwisho. Tazameni, malipo ya watendakazi-wale ambao hamjawalipa kwa kuvuna katika mashamba yenu- wanalia! Na kilio cha wale waliovuna mazao yenu kimeyafikia masikio ya Bwana wa Majeshi. Mmeishi kwa anasa duniani na kujifurahisha ninyi wenyewe. Mmejinenepesha mioyo yenu kwa siku ya machinjo. Mmemhukumu na kumuua mwenye haki asiyeweza kuwapinga. Kwa hiyo vumilieni, ndugu, mpaka ujio wa Bwana, kama mkulima husubiri mavuno ya thamani toka katika nchi, akisubiri kwa uvumilivu kwa ajili yake, mpaka mvua za kwanza na zile za mwisho zikinyesha. Pia ninyi muwe wavumilivu; kazeni mioyo yenu, kwa sababu kuja kwake Bwana ni karibu. Ndugu, msinung'unikiane ninyi kwa ninyi, kusudi msije mkahukumiwa. Tazama, hakimu anasimama mlangoni. 10 Kwa mfano, ndugu, angalieni mateso na uvumilivu wa manabii walionena katika jina la Bwana. 11 Tazama, twawaita wale wanaovumilia, “heri.” Mmesikia uvumilivu wa Ayubu, na mnalijua kusudi la Bwana kwa ajili ya Ayubu, ni kwa jinsi gani Bwana amejaa huruma na rehema. 12 Zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, aidha kwa mbingu ama kwa nchi, au kwa kiapo cha aina nyingine. Bali hebu “ndiyo” yenu na imaanishe “ndiyo” na “hapana” yenu na imaanishe “hapana,” ili kwamba msije kuangukia chini ya hukumu. 13 Kuna yeyote miongoni mwenu ana mateso? Lazima aombe. Je, mtu yeyote ni mwenye kuchangamka? Na aimbe sifa. 14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Na awaite wazee wa kanisa, nao wazee wa kanisa waombe juu yake, wakimpaka mafuta katika jina la Bwana, 15 na maombi ya imani yatamponya mgonjwa, na Bwana atamwinua. Na kama atakuwa ametenda dhambi, Mungu atamsamehe. 16 Kwa hiyo ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana kila mmoja na mwenzake, ili muweze kuponywa. Maombi ya mwenye haki huzaa matokeo makubwa. 17 Eliya alikuwa mtu mwenye hisia kama zetu, aliomba kwa juhudi kwamba mvua isinyeshe, na haikunyesha katika nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Na Eliya aliomba tena, na mbingu zilimwaga mvua juu ya nchi na nchi ikatoa mavuno. 19 Ndugu zangu, kama yeyote miongoni mwenu anapotoka kutoka kwenye ukweli, lakini mtu mwingine akamrejesha, 20 hebu na ajue kuwa yeyote amwongozaye mwenye dhambi kuondoka katika njia yake ya ukosaji ataponya nafsi yake kutoka katika mauti na atafunika wingi wa dhambi.