7
1 Lakini watu wa Israeli hawakutenda katika uaminifu kuhusiana na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya uharibifu. Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, kutoka katika kabila la Yuda, alivitwaa baadhi ya vitu hivyo vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili ya uharibifu, na hasira ya Yahweh iliwaka juu yawatu wa Israeli. 2 Yoshua alituma watu kutoka Yeriko kwenda Ai, mji uliokuwa karibu na Bethi Aveni, mashariki mwa Betheli. Aliwaambia, “Nendeni na mkaipeleleza nchi.” Wale watu walikwea na kuipeleleza Ai. 3 Waliporudi kwa Yoshua, walimwambia, “Usitume watu wote kwenda Ai. Tuma tu watu elfu mbili au elfu tatu waende kuiteka Ai. Usiwafanye watu wateseke katika vita, kwani ni watu wachache.” 4 Hivyo ni watu wapatao elfu tatu tu kutoka katika jeshi ndio walioenda, lakini watu hawa waliwakimbia watu wa Ai. 5 Watu wa Ai waliwaua watu wapatao thelathini na sita, waliwafuata katika lango la mji hadi katika machimbo ya mawe, na waliwauwa walipokuwa wakishuka katika kilima. Na mioyo ya watu ilijawa hofu na ujasiri wao ukawatoka. 6 Basi Yoshua alizirarua nguo zake. Yeye pamoja na wazewe wa Israeli waliweka mavumbi juu ya vichwa vyao na wakainamisha vichwa vyao hadi katika nchi mbele ya sanduku la Yahweh, na walibaki pale mpaka jioni. 7 Kisha Yoshua akasema, “Oo, Yahweh Bwana, kwanini umewavusha watu hawa ng'ambo ya Yordani? Kutuweka katika mikono ya Waamori ili kutuangamiza? ikiwa kama tulifanya maamuzi tofauti na tungekaa katika upande mwingine wa Yordani! 8 Bwana, niseme nini, baada ya Israeli kuwatega migongo maadui zao? 9 Kwa kuwa Wakaanani na wenyeji wote wa nchi watakaposikia, watatuzunguka na kuwafanya watu wa nchi kulisahau jina letu. Na utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu? 10 Yahweh akamwambia Yoshua, “Inuka! kwanini umelala kifudifudi? 11 Israeli imetenda dhambi. Wamevunja agano langu nililowaagiza. Wameiba baadhi ya vitu vilivyokuwa vimetengwa. Wameiba na kisha pia wakaficha dhambi yao kwa kuweka vitu vile walivyochukua miongoni mwa mali zao wenyewe. 12 Na matokeo yake ni kwamba watu wa Israeli hawataweza kusimama mbele za maadui zao. Walitega migongo yao kwa maadui zao kwasababu wao wenyewe wametengwa kwa ajili ya uharibifu. Sitakuwa pamoja nanyi tena mpaka pale mtakapoteketeza vitu vile vilivyotakiwa kuharibiwa, lakini sasa bado viko miongoni mwenu. 13 Inuka! Waweke watu wakfu kwangu, na uwaambie, 'Jiwekeeni wakfu ninyi wenyewe kesho. Kwa kuwa, Yahweh, Mungu wa Israeli asema hivi, “Kuna vitu vilitengwa ili kuteketezwa ambavyo bado viko miongoni mwenu, Israeli. Hamtaweza kusimama mbele ya maadui zenu mpaka pale mtakapoviondoa miongoni mwenu vitu vyote ambavyo vilitengwa kwa ajili ya kuteketezwa.” 14 Asubuhi, mtajisogeza wenyewe kwa makabila. Kabila lile ambalo Yahweh atalichagua litasogea karibu kwa koo zake. Ukoo ule ambao Yahweh atauchagua lazima usogee karibu kwa nyumba. Nyumba ambayo Yahweh ataichagua lazima isogee karibu kwa mtu mmoja mmoja. 15 Itakuwa hivi mtu yule atakayechaguliwa na aliye navyo vitu hivyo vilivyotengwa kwa ajili ya kuharibiwa, atachomwa moto, yeye na kila kitu alichonacho, kwasababu amelivunja agano la Yahweh na kwasababu amefanya jambo la aibu katika Israeli.'” 16 Basi, Yoshua aliamka asubuhi na mapema na aliwaleta Israeli karibu, kabila kwa kabila, na kabila la Yuda lilichaguliwa. 17 Yoshua akazisogeza koo za Yuda karibu, na ukoo wa Zera ulichaguliwa. Akausogeza karibu ukoo wa Zera mtu kwa mtu, na Zabdi alichaguliwa. 18 Akaisogeza karibu nyumba ya Zabdi mtu kwa mtu, na Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, kutoka kabila la Yuda, alichaguliwa. 19 Kisha Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, niambie ukweli mbele za Yahweh, Mungu wa Israel, na ufanye ukiri wako kwake. Tafadhali niambie kile ulichofanya. Usinifiche.” 20 Akani akamjibu Yoshua, “ Kwa kweli nimetenda dhambi mbele Yahweh, Mungu wa Israeli. 21 Nilichofanya ni hiki: Nilipoona miongoni mwa nyara mkoti mzuri kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kipande cha dhahabu chenye uzito wa shekeli hamsini, nilivitamani na nikavichukua. Vimefichwa chini ardhini katikati ya hema langu, na fedha iko chini yake.” 22 Yoshua akatuma wajumbe waliokimbia mpaka kwenye hema mahali palipokuwa na vile vitu. Walipoangalia, waliviona vimefichwa katika hema lake, na fedha chini yake. 23 Walivichukua vitu hivyo kutoka katikati ya hema na kuvileta kwa Yoshua na watu wote wa Israeli. Walivimwaga mbele za Yahweh. 24 Kisha Yoshua na Waisraeli wote pamoja naye, walimchukua Akani mwana wa Zera, na fedha, na koti, na kipande cha dhahabu, wana na binti zake, ng'ombe zake, punda zake, kondoo zake, hema lake, na kila kitu alichokuwa nacho, na wakavileta hata bonde la Akori. 25 Kisha Yoshua akasema, “Kwanini umetusumbua? Leo Yahweh atakutesa na wewe.” Waisraeli wote wakampiga kwa mawe. Na wakawachoma wote kwa moto, na wakawapiga mawe. 26 Kisha wakaweka juu yake kichuguu kikubwa cha mawe ambayo yapo hata leo. Yahweh akaachilia mbali hasira yake. Hivyo basi, jina la mahali hapo likawa Akori hata leo.