18
1 Kisha akawaambia mfano wa namna wanavyopaswa kuomba daima, na wasikate tamaa. 2 akaisema, 'Kulikuwa na hakimu katika mji fulani, ambaye hakuwa anamwogopa Mungu na hakuwaheshimu watu. 3 Kulikuwa na mjane katika jiji hilo, naye alimwendea mara nyingi, akisema, 'Nisaidie kupata haki dhidi ya mpinzani wangu.' 4 Kwa muda mrefu hakuwa tayari kumsaidia, lakini baada ya muda akasema moyoni mwake, `Ingawa mimi simwogopi Mungu au kuheshimu mtu, 5 lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua nitamsaidia kupata haki yake, ili asije akanichosha kwa kunijia mara kwa mara. '' 6 Kisha Bwana akasema, 'Sikiliza alivyosema huyo hakimu dhalimu. 7 Je Mungu pia hataleta haki kwa wateule wake ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, yeye hatakuwa mvumilivu kwao? 8 Nawaambia kwamba ataleta haki kwao upesi. Lakini wakati Mwana wa Adamu atakapokuja, je, atakuta imani duniani? ' 9 Ndipo akawaambia mfano huu kwa baadhi ya watu ambao wanajiona wenyewe kuwa wenye haki na kuwadharau watu wengine, 10 'Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo mwingine mtoza ushuru. 11 Farisayo akasimama akaomba mambo haya juu yake mwenyewe, 'Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine ambao ni wanyang'anyi, watu wasio waadilifu, wazinzi, au kama huyu mtoza ushuru. 12 Nafunga mara mbili kila wiki. Natoa zaka katika mapato yote ninayopata. ' 13 Lakini yule mtoza ushuru, alisimama mbali, bila hakuweza hata kuinua macho yake mbinguni, akagonga kifua chake akisema, 'Mungu, nirehemu mimi mwenye dhambi.' 14 Nawaambia, mtu huyu alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki kuliko yule mwingine, kwa sababu kila ajikwezaye atashushwa, lakini kila mtu anayejinyenyekeza atainuliwa. ' 15 Watu walimletea watoto wao wachanga, ili aweze kuwagusa, lakini wanafunzi wake walipoona hayo, wakawazuia. 16 Lakini Yesu akawaita kwake akisema, 'Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie. Maana ufalme wa Mungu ni wa watu kama hao. 17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto ni dhahiri hatauingia. ' 18 Mtawala mmoja akamwuliza, akisema, 'Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?' 19 Yesu akamwambia, 'Kwa nini unaniita mwema? Hakuna mtu aliye mwema, ila Mungu peke yake. 20 Unazijua amri- usizini, usiue, Usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako. 21 Yule mtawala akasema, 'Mambo haya yote nimeyashika tangu nilipokuwa kijana.' 22 Yesu alipoyasikia hayo akamwambia, '“Umepungukiwa jambo moja. Lazima uuze vyote ulivyonavyo na uwagawie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni -kisha njoo, unifuate. ' 23 Lakini tajiri aliposikia hayo, alihuzunika sana, kwa sababu alikuwa tajiri sana. 24 Kisha Yesu, akamwona alivyohuzunika sana akasema, 'Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! 25 Maana ni rahisi sana kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu. ' 26 Wale waliosikia hayo, wakasema, 'Nani basi, atakayeweza kuokolewa?' 27 Yesu akajibu, 'Mambo yasiyowezekana kwa mwanadamu kwa Mungu yanawezekana.” 28 Petro akasema, 'Naam, sisi tumeacha kila kitu na tumekufuata wewe. ' 29 Kisha Yesu akawaambia, Amin, nawaambia kwamba hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto, kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, 30 ambaye hatapokea mengi zaidi katika ulimwengu huu, na katika ulimwengu ujao, uzima wa milele. ' 31 Baada ya kuwakusanya wale kumi na wawibili, akawaambia, 'Tazama, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote ambayo yameandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Adamu yatakamilishwa. 32 Kwa maana atatiwa mikononi mwa watu wa Mataifa na atatendewa dhihaka na jeuri, na kutemewa mate. 33 Baada ya kumchapa viboko watamwua na siku ya tatu atafufuka. ' 34 Hawakuelewa mambo haya, na neno hili lilikuwa limefichwa kwao, na hawakuelewa mambo yaliyosemwa. 35 Ikawa Yesu ulipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya barabara akiomba msaada, 36 aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza nini kinatokea. 37 Wakamwambia kwamba Yesu wa Nazareti anapita. 38 Hivyo yule kipofu akalia kwa sauti, akisema, 'Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.' 39 wale waliokuwa wakitembea walimkemea huyo kipofu, wakamwambia anyamaze. Lakini yeye akazidi kulia kwa sauti, 'Mwana wa Daudi, unirehemu. 40 Yesu akasimama akaamuru mtu yule aletwe kwake. Kisha yule kipofu alipomkaribia, Yesu akamwuliza, 41 'Unataka nikufanyie nini?' Akasema, 'Bwana, nataka kuona.' 42 Yesu akamwambia, 'Upate kuona. Imani yako imekuponya. ' 43 Mara hiyo akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Walipoona hili, watu wote wakamsifu Mungu.