3
1 Katika siku zile Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Yuda akisema, 2 “Tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni u karibu.” 3 Kwa maana huyu ndiye aliyenenwa na nabii Isaya akisema, “sauti ya mtu aitaye kutoka jangwani; 'wekeni tayari njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.”' 4 Sasa Yohana alivaa manyoya ya ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. 5 Kisha Yerusalemu, Yuda yote, na eneo lote linalozunguka mto Yorodani wakaenda kwake. 6 Walikuwa wakibatizwa naye katika mto Yorodani huku wakitubu dhambi zao. 7 Lakini alipowaona wengi wa mafarisayo na masadukayo wakija kwake kubatizwa, akawaambia, ''Enyi uzao wa nyoka wenye sumu nani aliye waonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? 8 Zaeni matunda yaipasayo toba. 9 Na msifikiri na kusemezana miongoni mwenu, 'Tunaye Ibrahimu kama baba yetu.' Kwa kuwa nawaambieni Mungu anaweza kumwinulia Ibrahimu watoto hata kutoka katika mawe haya. 10 Tayari shoka limekwisha kuwekwa kwenye mzizi wa miti. Kwahiyo kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa kwenye moto. 11 Ninawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi nami sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 12 Na pepeto lake li mkononi mwake kusafisha kabisa uwanda wake na kuikusanya ngano yake ghalani. Lakini atayachoma makapi kwa moto ambao hauwezi kuzimika. 13 Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka mto Yorodani kubatizwa na Yohana. 14 Lakini Yohana alitaka kumzuia akisema, “Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?'' 15 Yesu akajibu akasema, ''Ruhusu iwe hivi sasa, kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote.'' Kisha Yohana akamruhusu. 16 Baada ya kuwa amebatizwa, mara Yesu alitoka kwenye maji, na tazama, Mbingu zikafunguka kwake. Na alimuona Roho wa Mungu akishuka kwa mfano wa njiwa na kutulia juu yake. 17 Tazama, sauti ilitoka mbinguni ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Ninaye pendezwa sana naye.''