12
1 Anayependa mafundisho hupenda maarifa, bali yule anayechukia maonyo ni mpumbavu. 2 Yehova humpa fadhila mtu mwema, bali mtu ambaye hufanya mipango ya ufisada atahukumiwa. 3 Mtu hawezi kuimarishwa kwa uovu, bali wale watendao haki hawawezi kung'olewa. 4 Mke mwema ni taji ya mume wake, bali yule aletaye aibu ni kama ugonjwa unaoozesha mifupa yake. 5 Mipango ya wale watendao haki ni adili, bali shauri la mwovu ni udanganyifu. 6 Maneno ya watu waovu ni uviziaji unaosubiri nafasi ya kuua, bali maneno ya mwenye haki yatawatunza salama. 7 Watu waovu wametupwa na kuondolewa, bali nyumba ya wale watendao haki itasimama. 8 Mtu husifiwa kwa kadri ya hekima yake, bali yule anayechagua ukaidi hudharauliwa. 9 Bora kuwa na cheo duni- kuwa mtumishi tu- kuliko kujisifu kuhusu ukuu wako bila kuwa na chakula. 10 Yule atendaye haki anajali mahitaji ya mnyama wake, bali huruma ya mwovu ni ukatili. 11 Yule atendaye kazi katika shamba lake atapata chakula tele, bali anayesaka miradi duni hana akili. 12 Watu waovu hutamani wanavyoiba watu wabaya kutoka kwa wengine, bali tunda la wale watendao haki hutoka kwao mwenyewe. 13 Mtu mbaya hunaswa kwa maongezi yake mabaya, bali wale watendao haki hujinasua katika taabu. 14 Mtu hushiba vitu vyema kutokana na tunda la maneno yake, kama vile kazi ya mikono yake inavyompa thawabu. 15 Njia ya mpumbavu ni sawa machoni pake mwenyewe, bali mtu wa hekima husikiliza ushauri. 16 Mpumbavu huonyesha hasira yake papo hapo, bali asiyejali tusi ni mwenye busara. 17 Asemaye ukweli huongea ilivyo haki, bali shahidi wa uongo huongea uongo. 18 Maneno yake asemaye kwa pupa ni kama kurusha upanga, bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji. 19 Midomo yenye kweli itadumu milele, bali ulimi wa uongo ni kwa kitambo kidogo tu. 20 Kuna udanganyifu katika mioyo ya wale wanaopanga kutenda uovu, bali furaha hutoka kwa washauri wa amani. 21 Hakuna ugonjwa utakaowajia wale watendao haki, bali watu waovu watajazwa matatizo. 22 Yehova anachukia midomo ya uongo, bali wale ambao huishi kwa uaminifu ndiyo furaha yake. 23 Mtu mwenye busara anasitiri maarifa yake, bali moyo wa wapumbavu hupiga yowe za kipumbavu. 24 Mkono wa mwenye bidii utatawala, bali watu wavivu watawekwa katika kazi za kulazimishwa. 25 Mashaka katika moyo wa mtu humwelemea, bali neno zuri humfurahisha. 26 Mwenye haki ni kiongozi kwa rafiki yake, bali njia ya waovu huwaongoza katika kupotea. 27 Watu wavivu hawawezi kubanika mawindo yao wenyewe, bali mtu wenye bidii atapata mali zenye thamani. 28 Wale ambao wanatembea katika njia ya haki wanapata uzima na katika mapito hayo hakuna kifo.