105
1 Mshukuruni Yahwe, liitieni jina lake; myafanye matendo yake yajulikane kati ya mataifa. 2 Mwimbieni yeye, mwimbieni sifa yeye; semeni matendo yake yote ya ajau. 3 Mjivune katika utakatifu wa jina lake; moyo wao wamtafutao Yahwe ufurahi. 4 Mtafuteni Yahwe na nguvu zake; utafuteni uwepo wake siku zote. 5 Kumbukeni mambo ya ajabu aliyoyatenda, 6 miujiza yake na amri zitokazo kinywani mwake, enyi kizazi cha Ibrahimu mtumishi wake, enyi watu wa Yakobo, wachaguliwa wake. 7 Yeye ni Yahwe, Mungu wetu. Amri zake ziko juu ya nchi yote. 8 Naye hulikumbuka agano lake milele, neno alilo amuru kwa ajili ya vizazi elfu. 9 Hulikumbuka agano alilolifanya na Ibrahimu na kiapo alicho mwapia Isaka. 10 Hiki ndicho alicho mthibitishia Yakobo kama agano na kama agano la milele kwa Israeli. 11 Alisema, “Nitakupa wewe ardhi ya Kanaani kama sehemu yako ya urithi.” 12 Alisema hili wakati tu walipokuwa wachache katika hesabu, yaani wachahe sana, nao walikuwa wageni katika nchi. 13 Walienda taifa hadi taifa na kutoka ufalme moja kwenda mwingine. 14 Hakuruhusu yeyote kuwaonea; aliwakemea wafalme kwa ajili yao. 15 Alisema, “Msiwaguze wapakwa mafuta wangu, na msiwadhuru manabii wangu.” 16 Aliita njaa katika nchi; akaondoa upatikanaji wa mkate wote. 17 Akatuma mtu mbele yao; Yusufu aliuzwa kama mtumishi. 18 Miguu yake ilifungwa kwa pingu; alivishwa mnyororo wa chuma shingoni mwake, 19 mpaka wakati wa maneno yake ulipotimia, nalo neno la Yahwe lilimjaribu. 20 Mfalme alituma watumishi kumfungua; mtawala wa watu alimuweka huru. 21 Alimuweka kuwa msimamizi wa nyumba yake kama mtawala wa mali zake zote 22 kuwaelekeza wakuu kama alivyopenda na kuwafundisha viongozi wake hekima. 23 Kisha Israeli iliingia Misri, na Yakobo aliishi kwa muda katika nchi ya Hamu. 24 Yahwe aliwajalia watu wake wazae sana, na aliwafanya wenye nguvu kuliko adui zao. 25 Alisababisha adui zao wawachukie watu wake, na kuwatendea visivyo watumishi wake. 26 Alimtuma Musa, mtumishi wake, na Haruni, ambaye alikwisha mchagua. 27 Walifanya ishara zake kati ya Wamisri na maajabu yake katika ya nchi ya Hamu. 28 Alituma giza na likaifanya nchi hiyo kuwa giza, lakini watu wake hawakutii amri zake. 29 Aligeuza maji kuwa damu na aliua samaki wao. 30 Nchi yao ilijaa vyura, hata katika vyumba vya watawala wao. 31 Alisema, na makundi ya inzi na chawa wakaja mjini mwote. 32 Aliigeuza mvua yao kuwa mvua ya mawe, pamoja na miali ya moto juu ya ardhi yao. 33 Aliiharibu mizabibu yao na mitini yao; akaivunja miti ya mji wao. 34 Alisema, na nzige wakaja, nzige wengi sana. 35 Nzige walikula mboga zao zote za majani katika nchi yao. Walikula mazao yote ardhini. 36 Aliua kila mzaliwa wa kwanza katika nchi yao, malimbuko ya nguvu zao. 37 Aliwatoa nje Waisraeli wakiwa na fedha na dhahabu; hakuna mmoja wa kabila lake aliyejikwaa njiani. 38 Misri ilifurahi walipoondoka, maana Wamisri waliwaogopa. 39 Alitandaza wingu liwafunike na alifanya moto uwaangazie wakati wa usiku. 40 Waisraeli waliomba chakula, naye aliwaletea kware na aliwatosheleza kwa mkate kutoka mbiguni. 41 Aliugawa mwamba, maji yalimwagika kutoka humo; yalitiririka katika jangwa kama mto. 42 Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu aliyoifanya kwa Ibrahimu mtumishi wake. 43 Aliwaongoza watu wake kwa furaha, wateule wake kwa kelele za ushindi. 44 Aliwapa nchi za mataifa; walichukua milki ya mali za watu 45 ili waweze kushika amri zake na kutii sheria zake. Msifuni Yahwe.