144
Zaburi ya Daudi. 1 Atukuzwe Yahwe, mwamba wangu, anifundishaye mikono yangu vita na vidole vyangu kupigana. 2 Wewe ni uaminifu wa agano langu na ngome yangu, mnara wangu mrefu na uniokoaye, ngao yangu na yule ambaye katika yeye napata kimbilio, uyatiishaye mataifa chini yangu. 3 Ee Yahwe, mtu ni kitu gani hata umtazame au mwana wa mtu hata umfikirie? 4 Mtu ni kama pumzi, siku zake ni kama uvuli upitao. 5 Ee Yahwe uziinamishe mbingu na ushuke chini, uiguse milima na uifanye kutoa moshi. 6 Utume umeme uwatawanye adui zangu; upige mishale yako na uwavuruge. 7 Nyosha mkono wako toka juu; uniokoe kutoka katika maji mengi, na kutoka katika mkono wa wageni. 8 vinywa vyao hunena uongo, na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo. 9 Nitakuimbia wimbo mpya, Mungu; kwa kinanda cha nyuzi kumi nitakuimbia sifa wewe, 10 uwapaye wafalme wokovu, uliye muokoa Daudi mtumishi wako dhidi ya upanga wa uovu. 11 Uniokoe na unitoe mkononi mwa wageni. Midomo yao huongea uongo, na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo. 12 Wana wetu na wawe kama mimea ikuayo kwa ukumbwa timilifu katika ujana wao na binti zetu kama nguzo za pembeni, zilizonakishiwa kwa kupamba jumba la kifahari. 13 Ghala zetu na zijae akiba ya kila aina ya mazao, na kondoo wetu wazae elfu na makumi elfu mashambani mwetu. 14 Kisha ng'ombe wetu watakuwa na nddama wengi. Hakuna atakayevunja kuta zetu; hakutakuwa na uhamisho wala kilio mitaani mwetu. 15 Wamebarikiwa watu wenye baraka hizo; furaha ina watu ambao Mungu wao ni Yahwe.