8
1 Wakati Mwanakondoo alipofungua muhuri ya saba, kukawa na ukimya mbinguni takribani nusu saa. 2 Kisha nikaona malaika saba wasimamao mbele za Mungu, na wakapewa tarumbeta saba. 3 Malaika mwingine akaja, ameshikilia bakuli ya dhahabu yenye uvumba, amesimama madhabahuni. Akapewa uvumba mwingi ili kwamba autoe pamoja na maombi ya waamini wote katika madhabahu ya dhahabu mbele ya kiti cha enzi. 4 Moshi wa ule uvumba, pamoja na maombi ya waamini, ukapanda juu mbele za Mungu kutoka mkononi mwa malaika. 5 Malaika akatwaa bakuli la uvumba na akalijaza moto kutoka kwenye madhabahu. Kisha akalitupa chini juu ya nchi, na kukatokea sauti za radi, miale ya radi na tetemeko la nchi. 6 Wale malaika saba ambao walikuwa na tarumbeta saba wakawa tayari kuzipiga. 7 Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, na kukatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyikana na damu. Vikatupwa chini katika nchi ili kwamba theluthi yake iungue, theluthi ya miti ikaungua na nyasi zote za kijani zikaungua. 8 Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake, na kitu kama mlima mkubwa uliokuwa unaungua kwa moto ukatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu, 9 theluthi ya viumbe hai katika bahari vikafa, na theluthi ya meli zikaharibiwa. 10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, ikimulika kama kurunzi, juu ya theluthi ya mito na chemichemi za maji. 11 Jina la nyota ni pakanga. Theluthi ya maji ikawa pakanga, na watu wengi wakafa kutokana na maji yaliyokuwa machungu. 12 Malaika wa nne alipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua ikapigwa, pamoja na theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota. Kwa hiyo theluthi ya vyote ikageuka kuwa giza; theluthi ya mchana na theluthi ya usiku havikuwa na mwanga. 13 Nilitazama, na nikasikia tai aliye kuwa anaruka katikati ya anga, akiita kwa sauti kuu, “Ole, ole, ole, kwa wale wakaao katika nchi, kwa sababu ya mlipuko wa tarumbeta iliyosalia ambayo imekaribia kupigwa na malaika watatu.”