21
Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa kuwa mbingu ya kwanza na nchi ya kwanza zimekwishapita, na bahari haikuwepo tena. Niliona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ambao ulikuja chini kutoka mbinguni kwa Mungu, ulioandaliwa kama bibi harusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. Nilisikia sauti kubwa kutoka kwenye kiti cha enzi ikisema, “Tazama! Makao ya Mungu yapo pamoja na wanadamu, naye ataishi pamoja nao. Watakuwa watu wake, na Mungu mwenyewe atakuwa nao na atakuwa Mungu wao. Atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na hapatakuwa na kifo tena, au kuomboleza, au kulia, au maumivu. Mambo ya zamani yamekwishakupita. Yeye ambaye alikuwa ameketi juu ya kiti cha enzi alisema, “Tazama! Nafanya mambo yote kuwa mapya.” Alisema, “Andika hili kwa sababu maneno haya ni ya hakika na kweli.” Aliniambia, “Mambo haya yalikwisha kupita! Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho. Kwa yeyote aonaye kiu nitampatia kinywaji bila gharama kutoka katika chemchemi za maji ya uzima. Yeye ashindaye atayarithi mambo haya, na nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Lakini kama ilivyo kwa waoga, wasioamini, wachukizao, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote, sehemu yao itakuwa katika ziwa la moto wa kiberiti uunguzao. Hiyo ndiyo mauti ya pili.” Mmoja wa malaika saba alikuja kwangu, mmoja ambaye alikuwa na mabakuli saba yaliyojaa mapigo saba ya mwisho na alisema, “Njoo hapa. Nitakuonesha bibi harusi, mke wa mwana kondoo.” 10 Kisha alinichukua mbali katika Roho kwenye mlima mkubwa na mrefu na alinionesha mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka chini kutoka mbinguni kwa Mungu. 11 Yerusalemu ulikuwa na utukufu wa Mungu, na uzuri wake ulikuwa kama kito cha thamani, kama jiwe la kioo safi la yaspi. 12 Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye milango kumi na miwili, pamoja na malaika kumi na wawili milangoni. Juu ya milango palikuwa pameandikwa majina ya makabila kumi na mawili ya wana wa Israeli. 13 Upande wa mashariki palikuwa na milango mitatu, upande wa kusini milango mitatu, upande wa kaskazini milango mitatu, na upande wa magharibi milango mitatu. 14 Kuta za mji zilikuwa na misingi kumi na miwili, na juu yake palikuwa na majina kumi na mawili ya mitume kumi na wawili wa Mwana Kondoo. 15 Mmoja aliyeongea nami alikuwa na kipimo cha fimbo iliyotengenezwa kwa dhahabu kwa ajili ya kupima mji, milango yake na kuta zake. 16 Mji uliwekwa ndani ya mraba; urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Alipima mji kwa kipimio cha fimbo, stadia 12, 000 kwa urefu (urefu wake, upana, na kimo vilifanana). 17 Vilevile alipima ukuta wake, unene wake ulikuwa dhiraa 144 kwa vipimo vya kibinadamu (ambavyo pia ni vipimo vya malaika). 18 Ukuta ulikuwa umejengwa kwa yaspi na mji wenye dhahabu safi, kama kioo safi. 19 Misingi ya ukuta ilikuwa imepambwa na kila aina ya jiwe la thamani. La kwanza lilikuwa yaspi, la pili lilikuwa yakuti samawi, la tatu lilikuwa kalkedon, la nne zumaridi, 20 la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolitho, la nane zabarajadi, la tisa yakuti ya manjano, la kumi krisopraso, la kumi na moja hiakintho, la kumi na mbili amethisto. 21 Milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili, kila mlango ulitengenezwa kutoka kwenye lulu moja. Mitaa ya mji ilikuwa dhahabu safi, ikionekana kama kioo safi. 22 Sikuona hekalu lolote ndani ya mji, kwa kuwa Bwana Mungu, ambaye anatawala juu ya vyote, na Mwana Kondoo ni hekalu lake. 23 Mji haukuhitaji jua au mwezi ili kungaza juu yake kwa sababu utukufu wa Mungu uliangaza juu yake, na taa yake ni Mwana Kondoo. 24 Mataifa watatembea kwa mwanga wa mji huo. Wafalme wa dunia wataleta fahari zao ndani yake. 25 Milango yake haitafungwa wakati wa mchana, na hapatakuwa na usiku pale. 26 Wataleta fahari na heshima ya mataifa ndani yake, 27 na hakuna kichafu kitakachoingia ndani yake. Wala yeyote ambaye afanyaye jambo lolote la aibu au udanganyifu hataingia, bali ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana Kondoo.