11
1 Igeni mfano wangu, kama ninavyouiga mfano wa Kristo.
Utaratibu Katika Kuabudu
2 Ninawasifu kwa kuwa mnanikumbuka katika kila jambo na kwa kushika mafundisho niliyowapa.
3 Napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu. 4 Kila mwanaume anayeomba au kutoa unabii akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. 5 Naye kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii pasipo kufunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake, kwani ni sawa na yeye aliyenyoa nywele. 6 Kama mwanamke hatajifunika kichwa chake, basi inampasa kunyoa nywele zake. Lakini kama ni aibu kwa mwanamke kukata au kunyoa nywele zake, basi afunike kichwa chake. 7 Haimpasi mwanaume kufunika kichwa chake kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na utukufu wa Mungu, lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. 8 Kwa maana mwanaume hakutoka kwa mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanaume. 9 Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume. 10 Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka juu yake.
11 Lakini katika Bwana, mwanamke hajitegemei pasipo mwanaume na mwanaume hajitegemei pasipo mwanamke. 12 Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu. 13 Hukumuni ninyi wenyewe: Je, inafaa kwa mwanamke kumwomba Mungu bila kufunika kichwa chake? 14 Je, maumbile ya asili hayatufundishi kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu? 15 Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake? Kwa maana mwanamke amepewa nywele ndefu ili kumfunika. 16 Kama mtu anataka kubishana juu ya jambo hili, sisi wala makanisa ya Mungu hatutambui desturi nyingine.
Matumizi Mabaya Ya Meza Ya Bwana
17 Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara. 18 Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. 19 Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu. 20 Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula, 21 kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa. 22 Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha!
Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana
(Mathayo 26:26-29; Marko 14:22-25; Luka 22:14-20)
23 Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Yesu, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate, 24 naye akiisha kushukuru, akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” 25 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.” 26 Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana mpaka ajapo.
Kushiriki Meza Ya Bwana Isivyostahili
27 Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana. 28 Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe. 29 Kwa maana mtu yeyote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, hula na kunywa hukumu juu yake mwenyewe. 30 Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa. 31 Lakini kama tungejichunguza wenyewe tusingehukumiwa. 32 Tunapohukumiwa na Bwana, tunaadibishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
33 Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo pamoja ili kula, mngojane. 34 Kama mtu akiwa na njaa, ale nyumbani kwake ili mkutanapo pamoja msije mkahukumiwa.
Nami nitakapokuja nitawapa maelekezo zaidi.