15
Abiya Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 13:1–14:1)
Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya akawa mfalme wa Yuda, naye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka binti Abishalomu.* Yaani Absalomu, maana yake Baba wa amani.
Alitenda dhambi zote baba yake alizotenda kabla yake; moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana Mungu wake kama moyo wa Daudi baba yake ulivyokuwa. Pamoja na hayo, kwa ajili ya Daudi, Bwana Mungu wake akampa taa katika Yerusalemu kwa kumwinua mwana atawale badala yake na kwa kuifanya Yerusalemu kuwa imara. Kwa kuwa Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana na hakushindwa kushika maagizo yote ya Bwana siku zote za uhai wake, isipokuwa katika habari ya Uria, Mhiti.
Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu wakati wote wa maisha ya Abiya. Kwa habari ya matukio mengine ya utawala wa Abiya na yote aliyofanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu. Naye Abiya akalala na baba zake akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake.
Asa Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 15:16–16:6)
Katika mwaka wa ishirini wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa akawa mfalme wa Yuda, 10 naye akatawala katika Yerusalemu miaka arobaini na mmoja. Bibi yake aliitwa Maaka binti Abishalomu.
11 Asa akatenda yaliyo mema machoni mwa Bwana, kama alivyokuwa ametenda Daudi baba yake. 12 Akawafukuza mahanithi wa mahali pa kuabudia miungu kutoka nchi na kuondoa sanamu zote ambazo baba zake walikuwa wametengeneza. 13 Hata akamwondoa bibi yake Maaka kwenye wadhifa wake kama mama malkia, kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni. 14 Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Bwana kikamilifu maisha yake yote. 15 Akaleta ndani ya Hekalu la Bwana fedha na dhahabu na vile vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.
16 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zote za utawala wao. 17 Mfalme Baasha wa Israeli akashambulia Yuda na kuweka ngome mji wa Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala kuingia nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.
18 Kisha Asa akachukua fedha yote na dhahabu iliyokuwa imeachwa katika hazina za Hekalu la Bwana na za jumba lake mwenyewe la kifalme. Akawakabidhi maafisa wake na kuwatuma kwa Ben-Hadadi mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Aramu, Yaani Shamu (ambayo leo ni Syria). aliyekuwa akitawala Dameski. 19 “Akasema na pawepo mkataba kati yangu na wewe, kama ulivyokuwepo kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, nimekuletea zawadi ya fedha na dhahabu. Sasa vunja mkataba wako na Baasha mfalme wa Israeli ili aniondokee mimi.”
20 Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Akaishinda miji ya Iyoni, Dani, Abel-Beth-Maaka na Kinerethi yote, pamoja na Naftali. 21 Wakati Baasha aliposikia hili, akaacha kuijenga Rama na akaenda kuishi Tirsa. 22 Kisha Mfalme Asa akatoa amri kwa Yuda yote, pasipo kumbagua hata mmoja, kubeba mawe na mbao kutoka Rama, ambazo Baasha alikuwa akitumia huko. Mfalme Asa akazitumia kujengea Geba iliyoko Benyamini na Mispa pia.
23 Kwa matukio yote ya utawala wa Asa, mafanikio yake yote, yote aliyofanya na miji aliyoijenga, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Katika uzee wake, hata hivyo, alipata ugonjwa wa miguu. 24 Kisha Asa akalala pamoja na baba zake na kuzikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Naye Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake.
Nadabu Mfalme Wa Israeli
25 Nadabu mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Asa wa Yuda, naye akatawala Israeli kwa miaka miwili. 26 Akafanya maovu machoni pa Bwana, akienenda katika njia za baba yake na katika dhambi yake, ambayo alisababisha Israeli kuifanya.
27 Baasha mwana wa Ahiya wa nyumba ya Isakari akafanya shauri baya dhidi yake, naye akamuua huko Gibethoni, mji wa Wafilisti, wakati Nadabu na Israeli yote walipokuwa wameuzingira. 28 Baasha akamuua Nadabu katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, naye Baasha akaingia mahali pake kuwa mfalme.
29 Mara tu alipoanza kutawala, aliua jamaa yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu yeyote aliyekuwa hai, bali aliwaangamiza wote, kulingana na neno la Bwana lililotolewa kupitia kwa mtumishi wake Ahiya Mshiloni, 30 kwa sababu ya dhambi alizokuwa amezitenda Yeroboamu na kusababisha Israeli kuzitenda, tena kwa sababu alimkasirisha Bwana, Mungu wa Israeli.
31 Kwa matukio mengine ya utawala wa Nadabu na yote aliyofanya, je hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 32 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli wakati wote wa utawala wao.
Baasha Mfalme Wa Israeli
33 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya akawa mfalme wa Israeli yote huko Tirsa, naye akatawala kwa miaka ishirini na minne. 34 Akatenda maovu machoni pa Bwana, akienenda katika njia za Yeroboamu na dhambi yake, ambayo alikuwa amesababisha Israeli kuitenda.

*15:2 Yaani Absalomu, maana yake Baba wa amani.

15:18 Yaani Shamu (ambayo leo ni Syria).