Zaburi.
129.
Wimbo wa kwenda juu. Wamenionea mno tangu ujana wangu; Israeli na aseme sasa: 
wamenionea mno tangu ujana wangu, lakini bado hawajanishinda. 
Wakulima wamelima mgongo wangu, na kufanya mifereji yao mirefu. 
Lakini Bwana ni mwenye haki; amenifungua toka kamba za waovu. 
Wale wote waichukiao Sayuni na warudishwe nyuma kwa aibu. 
Wawe kama majani juu ya paa, ambayo hunyauka kabla hayajakua; 
kwa hayo mvunaji hawezi kujaza vitanga vyake, wala akusanyaye kujaza mikono yake. 
Wale wapitao karibu na wasiseme, “Baraka ya Bwana iwe juu yako; tunakubariki katika jina la Bwana.”