25
Basi Samweli akafariki. Waisraeli wote wakakusanyika pamoja na kumwomboleza, na wakamzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Daudi akainuka na akashuka hadi jangwa la Parani. Kulikuwa na mtu mmoja huko Maoni, na mali zake zilikuwa huko Karmali. Mtu huyo alikuwa tajiri sana. Alikuwa na kondoo elfu tatu na mbuzi elfu moja. Naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake huko Karmeli. Na mtu huyo aliitwa Nabali, na jina la mke wake aliitwa Abigaili. Mwanamke huyo alikuwa mwenye busara na mzuri kwa sura. Lakini mwanaume alikwa mkaidi na mwovu katika mambo yake. Alikuwa wa uzao wa nyumba ya Kalebu. Daudi akasikia akiwa jangwani kwamba Nabali alikuwa akiwakata manyoya kondoo wake. Hivyo Daudi aliwatuma kwake vijana kumi. Akawaambia wale vijana, “Pandeni kwanda Karmeli, mwendeeni Nabali, na mkamsalimie kwa jina langu. Mtamwambia, 'Uishi katika baraka, Uwe na amani na nyumba yako iwe na amani, na wote ulionao wawe na amani. Nasikia kwamba unao wakata manyoya. Wachungaji wako walikuwa pamoja nasi, na hatukuwafanyia ubaya, na muda wote wakiwa Karmeli hawakupotelewa kitu chochote. Waulize vijana wako, nao watakuambia. Basi vijana wangu wapate kibali machoni pako, maana tumefika siku ya sherehe. Tafadhali utoe cho chote ulicho nacho mkononi kwa watumishi wako na kwa Daudi mwanao.'” Vijana wa Daudi walipofika, walimwambia Nabali yote haya kwa niaba ya Daudi na kisha wakasubiri. 10 Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Daudi ni nani? Na ni nani mwana wa Yese? Siku hizi wapo watumishi wengi wanaotoroka bwana zao. 11 Je, nichukue mkate wangu na maji yangu na nyama yangu ambayo nimewachinjia wakata manyoya wangu, na niwape watu wanaotoka nisikokujua?” 12 Hivyo vijana wa Daudi waligeuka na kurudi, nakumwambia kila kitu kilichosemwa. 13 Daudi akawaambia watu wake, “Kila mtu ajifunge upanga wake.” Kila mtu akajifunga upanga wake. Daudi naye pia akajifunga upanga wake. Yapata kama watu mia nne wakafuatana na Daudi, na wengine mia mbili walibaki kulinda mizigo yao. 14 Lakini kijana mmojawapo alimwambia Abigaili, mke wa Nabali akasema, “Daudi aliwatuma wajumbe kutoka jangwani waje wamsalimu bwana wetu, na yeye akawatukana. 15 Bado watu hawa walitutendea mema. Hatukudhurika na hatukupoteza chochote wakati wote tulipotembea nao tulipokuwa mbugani. 16 Walikuwa ukuta wetu usiku na mchana, wakati wote tulikuwa pamoja nao tukichunga kondoo. 17 Kwa hiyo tambua hili na zingatia utafanya nini, maana ubaya unamvizia bwana wetu, na utakuwa juu ya nyumba yake yote. Yeye ni mtu asiyefaa na hakuna awezaye kushauriana naye.” 18 Ndipo Abigaili akaharakisha na akachukuwa mikate mia mbili, chupa mbili za divai, kondoo watano waliokwisha andaliwa, vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu, na mikate mia mbili ya tini na akavipakia juu ya punda. 19 Akamwambia kijana wake, “Tangulia mbele yangu, nami nitakuja nyuma yako.” Lakini hakumwambia mmewe Nabali. 20 Alipokuwa akienda juu ya punda wake na kutelemka penye kificho cha mlima, Daudi na watu wake walishuka chini wakimwelekea Abigaili, naye akakutana nao. 21 Basi Daudi alikuwa amesema, “Hakika nimelinda bure vyote alivyonavyo mtu huyu huko nyikani, na vyote alivyonavyo hakuna kilichopotea, pamoja na hayo amenilipa mabaya badala ya mema. 22 Mungu na anitendee hivyo mimi, Daudi, pia iwe zaidi, iwapo nitamwacha hata mtu mmoja wa kwake akiwa hai ifikapo kesho asubuhi. 23 Abigaili alipomwona Daudi, aliharakisha na kushuka chini ya punda wake, akalala kifudifudi na kujiinamisha hadi chini. 24 Akamwangukia miguuni pake na kusema, “Juu yangu tu, bwana wangu, na uwe uovu. Tafadhali acha mjakazi wako aseme nawe, tena uyasikilize maneno ya mjakazi wako. 25 Nakusihi bwana wangu usimjali mtu huyu asiyefaa, Nabali, kwa maana kama jina lake lilivyo, ndivyo alivyo. Jina lake ni Nabali, na upumbavu uko pamoja naye. Lakini mimi mjakazi wako sikuwaona vijana wa bwana wangu, uliowatuma. 26 Sasa basi, bwana wangu, kama BWANA aishivyo, na kama unavyoishi, kwa kuwa BWANA amekuondoa kutoka kumwaga damu, na kuacha kulipiza kisasi kwa mkono mwenyewe, basi adui zako, na wale ambao wanatafuta kumfanyia uovu bwana wangu, wawe kama Nabali 27 Na sasa zawadi hii ambayo mjakazi wako ameileta kwa bwana wangu, na wapewe vijana ambao wanamfuata bwana wangu. 28 Tafadhali ulisamehe kosa la mjakazi wako, maana BWANA hakika atamfanyia bwana wangu nyumba imara, kwa sababu bwana wangu anapigana vita vya BWANA; na uovu hautaonekana ndani yako maadamu unaishi. 29 Na ingawa watu wangeinuka na kukuandama ili wakuue, bado uhai wa bwana wangu utafungwa katika furushi la walio hai na BWANA Mungu wako; na atayatupa maisha ya adui zako mbali, kama vile kutoka katika mfuko wa kombeo. 30 Na itakuwa, BWANA atakapokuwa amemtimizia bwana wangu mambo yote mazuri ambayo amekuahidi, na alivyokufanya kiongozi juu ya Israeli, 31 jambo hili halitakuwa huzuni kwako, wala chukizo moyoni kwa bwana wangu, kwa sababu hukumwaga damu bila sababu, na hujajilipizia kisasi. Na BWANA akikuletea mafanikio, umkumbuke mjakazi wako.” 32 Ndipo Daudi akamwambia Abigaili, “BWANA, Mungu wa Israeli, abarikiwe, aliyekutuma uonane na mimi leo. 33 Na hekima yako ibarikiwe, nawe umebarikiwa, kwa sababu leo umenizuia nisiwe na hatia ya kumwaga damu, na kutojilipizia kisasi kwa mkono wangu mwenyewe. 34 Kwa kweli, kama BWANA, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisikuumize, kama usinge harakisha kuja ukutane nami, kwa hakika kesho asubuhi asinge salia hata mtoto mmoja wa kiume kwa Nabali.” 35 Kwa hiyo Daudi akavipokea kutoka mkononi mwake vile alivyokuwa amemletea; akamwambia, “Nenda kwa amani hadi nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako na nimekubali.” 36 Abigaili akarudi kwa Nabali; tazama, alikuwa akifanya sherehe katika mji wake, kama sherehe ya mfalme; na moyo wa Nabali ulifurahi ndani yake, kwa sababu alikwa amelewa sana. Kwa hiyo hakumwambia chochote kabisa hadi kulipopambazuka 37 Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, basi mkewe akamwambia mambo hayo; moyo wake ukafa ndani yake, na akawa kama jiwe. 38 Ikawa baada ya siku kumi BWANA alimpiga Nabali naye akafa. 39 Naye Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “BWANA abarikiwe, aliyenichukulia hatua ya shutuma yangu kutoka mkono wa Nabali, na kumzuia mtumishi wake asifanye maovu. Na amemrudishia Nabali tendo la uovu juu ya kichwa chake mwenyewe.” Ndipo Daudi akawatuma watu wakaongee na Abigaili, ili amchukue awe mke wake. 40 Watumishi wake Daudi walipofika kwa Abigaili huko Karmeli, wakaongea naye na kusema, “Daudi ametutuma kwako tukuchukue hadi kwake uwe mke wake.” 41 Abigaili aliinuka, akainamisha uso chini, na akasema, “Tazama, mjakazi wako ni mtumwa aoshaye miguu ya watumishi wa bwana wangu.” 42 Akaharakisha na kuamka, akapanda punda akiwa na vijakazi wake watano waliofuatana naye; akawafuata wajumbe wa Daudi, na akawa mke wake. 43 Daudi pia alimchukua Ahinoamu wa Yezreeli akamwoa; wote wawili wakawa wake zake. 44 Wakati huo Sauli alikuwa amempa Palti, mwana wa Laishi mtu wa Galimu, Mikali, binti yake, aliyekuwa mke wa Daudi.