48
1 Ikawa baada ya mambo haya, mmojawapo akamwambia Yusufu, “Tazama, baba yako ni mgonjwa.” Hivyo akaondoka pamoja na wanawe wawili, Manase na Efrahimu. 2 Yakobo alipoambiwa, “Tazama, mwanao Yusufu amekuja kukuona,” Israeli akakusanya nguvu na kukaa juu ya kitanda. 3 Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani. Akanibariki na 4 kuniambia, 'Tazama, nitakupa uzao mwingi, na kukuzidisha. Nitakufanya kuwa kusanyiko la mataifa. Nitakupa nchi hii wewe na uzao wako kuwa milki ya milele.' 5 Na sasa wanao wawili, waliozaliwa kwako katika nchi ya Misri kabla sijaja Misri, ni wangu. Efrahimu na Manase watakuwa wangu, kama walivyo Rubeni na Simioni. 6 Watoto utakaowapata baada ya hapo ni wako; watahesabiwa katika majina ya ndugu zao katika urithi wao. 7 Lakini kwangu mimi, nilipokuja kutoka Padani, kwa uzuni yangu Raheli alikufa njiani katika nchi ya Kanaani, wakati kungalipo kitambo kwenda Efrathi. Nilimzika pale katika njia iendayo Efrathi” (ndio, Bethlehemu). 8 Israeli alipowaona wana wa Yusufu, akasema, “Ni nani hawa?” 9 Yusufu akamwambia baba yake, “Hawa ni wanangu, Mungu alionipa hapa:” Israeli akasema, “Walete kwangu, kwamba niwabariki.” 10 Basi macho ya Israeli yalikuwa yanashindwa kwa ajili ya umri wake, hivyo hakuweza kuona. Hivyo Yusufu akawasogeza karibu yake, na akawabusu na kuwakumbatia. 11 Israeli akamwambia Yusufu, “Sikutazamia kuuona uso wako tena, Lakini Mungu ameniruhusu kuwaona hata wanao.” 12 Yusufu akawaondoa kati ya magoti ya Israeli, na kisha akainama na uso wake juu ya nchi. 13 Yusufu akawachukua wote wawili, Efrahimu katika mkono wake wa kulia kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kulia kuelekea mkono wa kulia wa Israeli, na akawasogeza kwake. 14 Israeli akainua mkono wake wa kulia na kuuweka juu ya kichwa cha Efrahimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto juu ya kichwa cha Manase. Akaipishanisha mikono yake, kwani Manase ndiye alikuwa mzaliwa wa kwanza. 15 Israeli akambariki Yusufu, akisema, Mungu ambaye mbele zake baba zangu Ibrahimu na Isaka walitembea, Mungu aliyenilinda hata leo, 16 malaika walionilinda na madhara yote, awabariki vijana hawa. Jina langu na litajwe kwao, na majina ya baba zangu Ibrahimu na Isaka. Na wawe makutano ya watu juu ya nchi.” 17 Yusufu alipoona baba yake ameweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Efrahimu, haikumpendeza. Akauchukuwa mkono wa baba yake auweke katika kichwa cha Manase. 18 Yusufu akamwambia baba yake, “Sivyo babangu; kwani huyu ndiye mzaliwa wa kwanza. Uweke mkono wako juu ya kichwa chake.” 19 Baba yake akakataa na kusema, “Ninafahamu, mwanangu, nafahamu. Yeye naye atakuwa watu, naye pia atakuwa mkuu. Lakini mdogo wake atakuwa mkuu kuliko yeye, na uzao wake utakuwa wingi wa mataifa.” 20 Israeli akawabariki siku hiyo kwa maneno haya, “Watu wa Israeli watatamka baraka kwa majina yenu wakisema, Mungu na akufanye kama Efrahimu na kama Manase'. “Kwa njia hii, Israeli akamweka Efrahimu mbele ya Manase. 21 Israeli akamwambia Yusufu, “Tazama, ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu. 22 Kwako wewe, kwa kuwa uko juu ya ndugu zako, ninakupa mtelemko wa mlima niliouchukuwa kutoka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.”