9
1 Wakati, kama Yesu alipokuwa akipita, alimwona mtu kipofu tangu kuzaliwa kwake. 2 Wanafunzi wake wakamwuliza, “Rabi, nani aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?” 3 Yesu akawajibu, “Siyo huyu mtu wala wazazi wake waliotenda dhambi, bali kazi za Mungu zipate kufunuliwa kupitia kwake. 4 Tunapaswa kufanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana. Usiku waja wakati ambapo hakuna atakayeweza kufanya kazi. 5 Wakati niwapo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.” 6 Baada ya Yesu kusema maneno haya, alitema kwenye ardhi, alifanya tope kwa mate, na akampaka yule mtu machoni na lile tope. 7 Akamwambia, nenda kaoge katika kisima cha Siloam (Inayotafsiriwa kama 'aliyetumwa').” Kwa hiyo huyo mtu alienda, akanawa, na akarudi, anaona. 8 Majirani wa yule mtu na wale waliomuona mwanzo kama mwombaji walisema, Je! huyu siye yule mtu aliyekuwa akikaa na kuomba?” wengine walisema, “Ni yeye.” 9 Na wengine walisema, “Hapana, bali anafanana naye.” Lakini alikuwa akisema, “Ni mimi.” 10 Wakamwambia, “Sasa macho yako yalifunguliwaje?” 11 Alijibu, mtu aitwaye Yesu alifanya tope na kupaka macho yangu na kuniambia, 'Nenda Siloam ukanawe.' Kwa hiyo nilienda, na nikanawa, na nikapata kuona tena.” 12 Wakamwambia, “Yuko wapi?” Alijibu, “Sijui.” 13 Wakampeleka yule mtu aliyewahi kuwa kipofu kwa Mafarisayo. 14 Nayo ilikuwa siku ya Sabato wakati Yesu alipotengeneza tope na kuyafumbua macho yake. 15 Ndipo tena Mafarisayo wakamwuliza alipataje kuona. Aliwaambia, “Aliweka tope katika macho yangu, nikanawa, na sasa naweza kuona.” 16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Mtu huyu hajatoka kwa Mungu kwa sababu haishiki Sabato.” Wengine walisema, “Inawezekanaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo?” Kwa hiyo kukawa na mgawanyiko kati yao. 17 Ndipo walipomwuliza yule kipofu tena, “Unasemaje juu yake kwa sababu aliyafungua macho yako?” Kipofu akasema, “Ni nabii.” 18 Hata wakati huu Wayahudi hawakumwamini kwamba alikuwa kipofu naye amepata kuona mpaka walipowaita wazazi wake yeye aliyepata kuona. 19 Waliwauliza wazazi, Je, huyu ni mtoto wenu mnayesema alizaliwa kipofu? amewezaje sasa kuona?” 20 Hivyo wazazi wake wakamjibu, “Tunajua kuwa huyu ni mtoto wetu na kwamba alizaliwa kipofu. 21 Jinsi gani sasa anaona, hatujui, na yeye aliyemfumbua macho yake, hatumjui. Mwulizeni yeye. Ni mtu mzima. Anaweza kujieleza mwenyewe.” 22 Wazazi wake walisema mambo haya, kwa sababu waliwaogopa Wayahudi. Kwa vile Wayahudi walikuwa wamekubaliana tayari kuwa, ikiwa yeyote atakiri kuwa Yesu ni Kristo, atatengwa na Sinagogi. 23 Kwa sababu hii, wazazi wake walisema, “Ni mtu mzima, mwulizeni yeye.” 24 Kwa hiyo kwa mara ya pili, walimwita yule mtu aliyewahi kuwa kipofu na kumwambia, “Mpe Mungu utukufu. Tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi.” 25 Ndipo yule mtu alijibu, “Awe ni mwenye dhambi, mimi sijui. Kitu kimoja ninachokijua: nilikuwa kipofu, na sasa ninaona.” 26 Ndipo walipomwambia, “Amekufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?” 27 Alijibu, “Nimekwishawaambia tayari, na nyinyi hamkusikiliza! Kwa nini mnataka kusikia tena? Nanyi hamtaki kuwa wanafunzi wake pia, sivyo? 28 Walimtukana na kusema, “Wewe ni mwanafunzi wake, lakini sisi ni wanafunzi wa Musa. 29 Tunajua kwamba Mungu alizungumza na Musa, lakini kwa huyu mtu, hatujui kule atokako.” 30 Yule mtu akajibu na kuwaambia, “Kwa nini, hili ni jambo la kushangaza, kwamba hamjui anakotoka, na bado ameyafumbua macho yangu. 31 Tunajua kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini ikiwa mtu yeyote anamwabudu Mungu na hufanya mapenzi yake, Mungu humsikiliza. 32 Tangu kuanza kwa Ulimwengu haijawahi kamwe kusikiwa kwamba yeyote ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. 33 Ikiwa mtu huyu hakutoka kwa Mungu, asingelifanya chochote.” 34 Walijibu na kumwambia, “Ulizaliwa katika dhambi kabisa, na wewe unatufundisha sisi?” Ndipo walipomfukuza kutoka katika sinagogi. 35 Yesu alisikia kwamba wamemwondoa kwenye sinagogi. Alimpata na kumwambia, “Unamwamini Mwana wa Mtu?” 36 Alijibu na kusema, “Ni nani, Bwana, ili nami nipate kumwamini?” 37 Yesu akamwambia, “Umeshamuona, naye unayezungumza naye ndiye.” 38 Yule mtu akasema, “Bwana, Naamini.” Ndipo akamsujudia. 39 Yesu akasema, “Kwa hukumu nimekuja katika Ulimwengu huu ili kwamba wale wasioona wapate kuona na wale wanaoona wawe vipofu.” 40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye wakasikia maneno hayo na kumwuliza, “Na sisi pia ni vipofu?” 41 Yesu akawaambia, “Kama mngelikuwa vipofu, msingelikuwa na dhambi. Hata hivyo, sasa mnasema, 'Tunaona,' dhambi yenu inakaa.”