Zaburi.
5.
Sikiliza nikuitapo, Yahweh; tazama kuugua kwangu. 
Sikiliza sauti yangu nikuitapo, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa kuwa ni kwako Bwana naomba. 
Yahweh; sikia kilio changu asubuhi; na asubuhi nitaleta dua yangu kwako na kungoja kwa matarajio. 
Hakika wewe ni Mungu usiye kubaliana na uovu; watu waovu hawawezi kuwa wageni wako. 
Wenye kiburi hawata simama katika uwepo wako; wewe unawachukia wote wanaofanya maovu. 
Nawe utawaharibu waongo; Yahweh huwadharau vurugu na watu wadanganyifu. 
Lakini kwangu mimi, kwa sababu ya ukuu na uaminifu wa agano lako, nitakuja nyumbani mwako; na kwa heshima nitakuinamia mbele ya hekalu lako takatifu. 
Oh Bwana, uniongoze katika haki yako kwa sababu ya adui zangu; usawazishe njia yako mbele yangu. 
Kwa kuwa midomoni mwao hamna ukweli; utu wao wa ndani ni mwovu; makoo yao ni kaburi lililo wazi; husifu kinafiki kwa ulimi wao. 
Mungu, wafanye kuwa na hatia; mipango yao iwe kuanguka kwao! Kwa ajili ya makosa yao mengi uwatoe nje, kwa kuwa wamekuasi wewe. 
Bali wale wanao kukimbilia wafurahi; uwafanye wapige kelele kwa shangwe siku zote kwa sababu unawapigania; uwafanye wenye furaha ndani yako, wale walipendao jina lako. 
Kwa maana utawabariki wenye haki, Yahweh; utawazunguka kwa neema kama ngao.