Zaburi. 119. Wamebarikiwa wale ambao njia zao hazina lawama, waenendao katika sheria ya Yahwe. Wamebarikiwa wale wazishikao amri zake thabiti, wamtafutao kwa moyo wao wote. Hawatendi makosa; wanaenenda katika njia zake. Wewe umetuamuru kuyashika maagizo yako ili tuyachunguze kwa umakini. Oh, ningependa njia zangu ziwe thabiti nizitii amri zako! Ndipo sitaaibika nizifikiripo amri zako zote. Nitakushukuru wewe kwa unyofu wangu wa moyo nijifunzapo amri za haki yako. Nitazitii amri zako; usiniache peke yangu. BETH. Ni jinsi gani kijana aweza kuendelea kuishi katika njia yake ya utakatifu? Ni kwa kulitii neno lako. Kwa moyo wangu wote ninakutafuta wewe; Usiniache nipotee mbali na maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka neno lako ili nisije nikakutenda dhambi. Umetukuka, Yahwe; unifundishe amri zako. Kwa kinywa changu nimetangaza amri ya haki yako yote ambayo umeifunua. Ninafurahi katika njia ya amri za agano lako zaidi kuliko katika utajiri. Nitayatafakari maagizo yako na kuzitilia maanani njia zako. Ninafurahia katika amri zako; sitalisahau neno lako. GIMEL. Uwe mwema kwa mtumishi wako ili niweze kuishi na kulishika neno lako. Ufungue macho yangu ili niweze kuona mambo ya ajabu katika sheria yako. Mimi ni mgeni katika nchi; usizifiche amri zako mbali nami. Moyo wangu unauma kwa kutamani sana kuzijua amri zako za haki wakati wote. Wewe huwakemea wenye kiburi, waliolaaniwa, wanao tanga-tanga mbali na amri zako. Uniokoe dhidi ya aibu na udhalilishaji, maana nimezitii amri za agano lako. Ingawa watawala wanapanga njama na kunikashfu, mtumishi wako huzitafakali amri zako. Amri za agano lako ni furaha yangu, na washauri wangu. DALETH. Uhai wangu unashikamana na mavumbi! nipe uhai kwa neno lako. Nilikuambia mapito yangu, na ulinijibu; nifundishe sheria zako. Unifahamishe njia ya maagizo yako, ili niweze kutafakari juu ya mafundisho yako ya ajabu. Nimelemewa na huzuni! Nitie nguvu kwa neno lako. Uiondoe kwangu njia ya udanganyifu; kwa wema wako unifundishe sheria yako. Nimechagua njia ya uaminifu; siku zote nimeweka amri za haki yako mbele yangu. Ninashikamana na amri za agano lako; Yahwe, usiniache niaibike. Nitakimbia katika njia ya amri zako, kwa sababu wausukuma moyo wangu kufanya hivyo. HE Unifundishe, Yahwe, njia za sheria yako, nami nitazishika hadi mwisho. Unipe uelewa, nami nitazishika sheria zako; nitazitii kwa moyo wangu wote. Uniongoze katika njia ya amri zako, maana ninafurahi kuenenda katika hizo. Uelekeze moyo wangu kuzielekea amari za agano lako na uniweke mbali na matendo yasiyo haki tena. Uyageuze macho yangu dhidi ya kutazama mambo yasiyofaa; unihuishe katika njia zako. Umtendee mtumishi wako ahadi ambayo uliifanya kwa wale wanaokuheshimu wewe. Uniondolee shutumu niiogopayo, maana hukumu zako za haki ni njema. Tazama, nimeyatamani maagizo yako; unihuishe katika haki yako. VAV. Ee Yahwe, unipe upendo wako usiokwisha na wokovu wako kulingana na ahadi yako; ndipo nitakuwa na jibu kwa ajili ya yule anayenidhihaki. Usiliondoe neno la kweli mdomoni mwangu, maana nimesubiri kwa ajili ya amri zako za haki. Nitazitii sheria zako siku zote, milele na milele. Nitaenenda salama, maana ninayatafuta maagizo yako. Nitazinena amri zako thabiti mbele ya wafalme nami sitaaibika. Ninafurahia katika amri zako, nizipendazo sana. Nitaziinulia mikono yangu amri zako, nizipendazo; nitazitafakari sheria zako. ZAYIN. Kumbuka ahadi yako kwa mtumishi wako kwa sababu umenipa tumaini. Hii ni faraja yangu katika mateso: kuwa ahadi yako imeniweka hai. Wenye kiburi wamenicheka, lakini sijaiacha sheria yako. Nimezitafakari amri zako za haki tangu zamani, Yahwe, nami ninajifariji mwenyewe. Hasira kali imenishikilia kwa sababu ya waovu wanaoikataa sheria yako. Sheria zako zimekuwa nyimbo zangu katika nyumba ninayoishi kwa muda. Ninalifikiria jina lako wakati wa usiku, Yahwe, na kuzishika sheria zako. Hili limekuwa zoezi langu kwa sababu nimeyatii maagizo yako. HETH. Yahwe ni sehemu yangu; nimeamua kuyatii maneno yake. Kwa bidii ninaomba neema yako kwa moyo wangu wote; unihurumie, kama neno lako lilivyo ahidi. Nilizichunguza njia zangu na kugeuzia miguu yangu kwenye amri za agano lako. Naharakisha na sichelewi kuzishika amri zako. Kamba za waovu zimenifunga; nami sijaisahau sheria yako. Katikati ya usiku ninaamka kukushukuru wewe kwa sababu ya amri za haki yako. Ninaurafiki na wale wanao kuabudu wewe, wale wote watiio maagizo yako. Yahwe, nchi, imejaa uaminifu wa agano lako; unifundishe sheria zako. TETH. Wewe umemtendea mema mtumishi wako, Yahwe, sawasawa na neno lako. Unifundishe utambuzi sahihi na uelewa, kwa kuwa nimeamini katika amri zako. Kabla sijateswa nilipotea, lakini sasa nimelitii neno lako. Wewe ni mwema, na ndiye yule utendaye mema; unifundishe sheria zako. Wenye kiburi wamenichafua kwa uongo, lakini niliyashika maagizo yako kwa moyo wangu wote. Mioyo yao ni migumu, lakini ninafurahia katika sheria yako. Ni vizuri kwangu kuwa nimeteseka ili niweze kujifunza sheria zako. Maagizo yatokayo kinywani mwako ni ya thamani zaidi kwangu kuliko maelfu ya vipande vya dhahabu na fedha. YOD. Mikono yako imeniumba na kunitengeneza; unipe uelewa ili niweze kujifunza amri zako. Wale wanao kucha wewe watafurahi wanionapo kwa sababu ninapata tumaini katika neno lako. Ninajua, Yahwe, kuwa amri zako ni za haki, na kuwa katika uaminifu ulinitesa. Agano lako aminifu na linifariji, kama ulivyomwahidi mtumishi wako. Unihurumie ili niweze kuishi, kwa maana sheria yako ni furaha yangu. Wenye kiburi na waaibishwe, maana wamenitukana; bali mimi nitayatafakari maagizo yako. Wale wote wanao kucha wewe na wanigeukie, wale wazijuao amri za agano lako. Moyo wangu uwe mkamilifu pamoja na heshima kwa sheria zako ili nisiaibike. KAPH. Ninazimia kwa kutamani sana kuwa wewe unaweza kuniokoa! Ninamatumaini katika neno lako. Macho yangu yanatamani sana kuiona ahadi yako; ni lini utanifariji mimi? Kwa maana nimekuwa kama kiriba katika moshi; sisahau sheria zako. Ni kwa muda gani gani mtumishi wako atalazimika kuyavumilia haya; ni lini utawahukumu wale wanaonitesa? Wenye kiburi wamenichimbia shimo, wasiotii sheria yako. Amri zako zote ni za kuaminika; wale watu walinitesa bila ya haki; unisaidie. karibu kunifanya nifikie mwisho juu ya nchi hii, lakini siyakatai maagizo yako. Kwa upendo wako thabiti, uniweke hai, ili niweze kuzitii amri zako. LAMEDH. Yahwe, neno lako linasimama milele; neno lako limefanywa imara mbinguni. Uaminifu wako wadumu kwa ajili ya vizazi vyote; umeiimarisha nchi, nayo inadumu. Vitu yote yaliendelea mpaka leo hii, kama vile ulivyosema katika amri zako za haki, maana vitu vyote ni watumishi wako. Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu, ningeangamia katika mateso yangu. Sitayasahau kamwe maagizo yako, maana kupitia hayo umeniweka hai. Mimi ni wako, kwa maana ninayatafuta maagizo yao. Waovu hujiandaa kuniangamiza, lakini nitatafuta kuzielewa amri za agano lako. Nimeona kuwa kila kitu kina mipaka, lakini amri zako ni pana, zaidi ya mipaka. MEM. Oh ni jinsi gani naipenda sheria yako! Ni tafakari yangu mchana kutwa. Amri zako hunifanya mwenye hekima kuliko adui zangu, maana amri zako siku zote ziko pamoja nami. Ninauelewa zaidi kuliko walimu wangu wote, kwa maana ninazitafakari amri za agano lako. Ninaelewa kuliko wale wanaonizidi umri; hii ni kwa sababu nimeyashika maagizo yako. Nimeiepusha miguu yangu na kila njia ya uovu ili niweze kulitii neno lako. Sijaenda kinyume na amri zako za haki, kwa maana wewe umenifundisha. Ni jinsi gani maneno yako ni matamu kwenye majaribu yangu, naam, matamu kuliko asali kinywani mwangu! Kupitia maagizo yako ninapata utambuzi; kwa hiyo kila njia isiyo ya kweli. Neno lako ni taa ya mguu miguu yangu na mwanga wa njia yangu. Nimeapa na nimethibitisha, kuwa nitazitii amri za haki yako. Nimeteswa sana; uniweke hai, Yahwe, kama ulivyoahidi katika neno lako. Yahwe, tafadhali pokea dhabihu yangu ya hiari ya kinywa changu, na unifundishe amri zako za haki. Uhai wangu ziku zote uko mkononi mwangu, lakini bado sisahau sheria yako. Waovu wamenitegea mtego, lakini sijapotea mbali na maagizo yako. Nimezifanya amri za agano lako kama urithi wangu milele, maana hizo ni furaha ya moyo wangu. Moyo wangu umewekwa kuzitii sheria zako milele mpaka mwisho kabisa. SAMEKH. Ninawachukia watu wa kusita-sita, lakini naipenda sheria yako. Wewe ni ficho langu na ngao yangu; nalingoja neno lako. Ondokeni kwangu, ninyi mtendao uovu, ili niweze kuzitii amri za Mungu wangu. Uniwezeshe kwa neno lako ili niweze kuishi na nisiaibike na matumaini yangu. Unisaidie, nami nitakuwa salama; siki zote nitazitafakari sheria zako. Wewe huwakataa wale wote wapoteao mbali na sheria zako, maana watu hao ni wadanganyifu na si wakuaminika. Wewe huwaondoa waovu wa nchi kama takataka; kwa hiyo ninazipenda amri zako thabiti. Mwili wangu hutetemeka kwa hofu yako, na ninaziogopa amri za haki yako. AYIN. Ninafanya kilicho sahihi na haki; usiniache kwa watesi wangu. Uwe mdhamini wa ustawi wa mtumishi wako; usiwaache wenye kiburi wanionee. Macho yangu yanachoka kwa kuusubiri wokovu wako na neno lako la haki. Mwoneshe mtumishi wako uaminifu wa agano lako, na unifundishe sheria zako. Mimi ni mtumishi wako; unipe uelewa ili niweze kuzijua amri za agano lako. Ni wakati wa Yahwe kutenda, kwa maana watu wamevunja sheria yako. Hakika ninazipenda amri zako kuliko dhahabu, naam, kuliko dhahabu safi. Hivyo ninayafuata maagizo yako yote kwa makini, na ninachukia kila njia ya uongo. PE. Sheria zako ni za ajabu, ndiyo sababu ninazitii. Ufafanuzi wa maneno yako huleta nuru; na kumpa ufahamu mjinga. Ninafungua kinywa changu na kutweta, maana ninazitamani amri zako. Unigeukie na unihurumie, kama ufanyavyo siku zote kwa wale walipendao jina lako. Uziongoze hatua zangu kwa neno lako; usiruhusu dhambi yeyote initawale. Unikomboe dhidi ya wanadamu waonevu ili niyatii maagizo yako. Uso wako umwangazie mtumishi wako, na unifundishe sheria zako. Mito ya machozi yatiririka kutoka machoni pangu kwa sababu watu hawaitii sheria yako. TSADHE. Wewe ni mwenye haki, Yahwe, na amri zako ni haki. Umezipa amri za agano lako haki na uaminifu. Hasira imeniangamiza kwa sababu adui zangu husahau maneno yako. Neno lako limepimwa sana, naye mtumishi wako analipenda. Sina umuhimu na ninadharauliwa, lakini bado siyasahau maagizo yako. Hukumu yako ni ya haki milele, na sheria yako ni ya kuaminika. Japo dhiki na taabu vimenipata, amri zako bado ni furaha yangu. Amri za agano lako ni za haki milele; unipe uelewa ili niweze kuishi. QOPH. Nililia kwa moyo wangu wote, “Unijibu, Yahwe, nitazishika sheria zako. Ninakuita wewe; uniokoe, nami nitazitii amri za agano lako.” NInaamka asubuhi kabla jua halijachomoza na kulia kwa ajili ya msaada. Ninatumaini katika maneno yako. Macho yangu yako wazi usiku kucha ili niweze kutafakari juu ya neno lako. Sikia sauti yangu katika uaminifu wa agano lako; uniweke hai, Yahwe, kama ulivyoahidi katika amri zako za haki. Wale wanaonitesa wananikaribia, lakini wako mbali na sheria yako. Wewe uko karibu, Yahwe, na amri zako ni za kuaminika. Muda mrefu uliopita nilijifunza kutoka katika amri za agano lako ulizoziweka katika mahali pa milele. RESH. Uyatazame mateso yangu na unisaidie, maana siisahau sheria yako. Unitetee na kunikomboa; unihifadhi, kama ulivyo ahidi katika neno lako. Wokovu uko mbali na waovu, maana hawazipendi amri zako. Matendo yako ya huruma ni makuu, Yahwe; uniweke hai; kama ufanyavyo siku zote. Watesi wangu na adui zangu ni wengi, lakini bado sijaenda mbali na amri za agano lako. Nimewaona wasaliti wakitia kinyaa kwa sababu hawalishiki neno lako. Tazama jinsi niyapendavyo maagizo yako; uniweke hai, Yahwe, kama ulivyoahidi katika uaminifu wa agano lako. Kiini cha neno lako ni kweli; kila mmoja mwenye amri za haki hudumu milele. SHIN. Wakuu hunitesa bila sababu; moyo wangu hutetemeka, ukiogopa kutolitii neno lako. Ninalifurahia neno lako kama apataye nyara nyingi. Ninachukia na kudharau uongo, lakini naipenda sheria yako. Mara saba kwa siku ninakusifu wewe kwa sababu ya amri zako za haki. Wana amani nyingi, waipendao sheria yako; hakuna cha kuwatia mashakani. Naungoja wokovu wako, Yahwe, na ninatii amri zako. Ninazishika amri zako thabiti, na ninazipenda sana. Ninayashika maagizo yako na amri zako thabiti, kwa maana unajua kila kitu nifanyacho. TAV. Sikia kilio changu, Yahwe; unipe uelewa wa neno lako. Maombi yangu yaje mbele zako; unisaidie, kama ulivyoahidi katika neno lako. Midomo yangu na imwage sifa, maana wewe unanifundisha sheria zako. Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako, maana amri zako zote ni za haki. Mkono wako unisaidie, maana nimechagua maagizo yako. Ninautamani wokovu wako, Yahwe, na sheria yako ni furaha yangu. Naomba niishi na nikusifu wewe, na amri zako za haki zinisaidie. Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; mtafute mtumishi wako, kwa maana sijazisahau amri zako.