Zaburi 88
Kilio Kwa Ajili Ya Kuomba Msaada
Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi leanothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi.
Ee Bwana, Mungu uniokoaye,
nimelia mbele zako usiku na mchana.
Maombi yangu yafike mbele zako,
utegee kilio changu sikio lako.
 
Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu,
na maisha yangu yanakaribia kaburi.* Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.
Nimehesabiwa miongoni mwa wale waendao shimoni,
niko kama mtu asiye na nguvu.
Nimetengwa pamoja na wafu,
kama waliochinjwa walalao kaburini,
ambao huwakumbuki tena,
ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako.
 
Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana,
katika vina vya giza nene.
Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu,
umenigharikisha kwa mawimbi yako yote.
 
Umenitenga na rafiki zangu wa karibu
na kunifanya chukizo kwao.
Nimezuiliwa, wala siwezi kutoroka;
nuru ya macho yangu
imefifia kwa ajili ya huzuni.
 
Ee Bwana, ninakuita kila siku,
ninakunyooshea wewe mikono yangu.
10 Je, wewe huwaonyesha wafu maajabu yako?
Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu?
 
11 Je, upendo wako hutangazwa kaburini,
uaminifu wako katika Uharibifu? Yaani Abadon.
12 Je, maajabu yako hujulikana mahali pa giza,
au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu?
 
13 Lakini ninakulilia wewe, Ee Bwana, unisaidie;
asubuhi maombi yangu huja mbele zako.
14 Ee Bwana, kwa nini unanikataa
na kunificha uso wako?
 
15 Tangu ujana wangu nimeteseka, nikakaribia kifo;
nimepatwa na hofu zako, nami nimekata tamaa.
16 Ghadhabu yako imepita juu yangu;
hofu zako zimeniangamiza.
17 Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko;
zimenimeza kabisa.
18 Umeniondolea marafiki na wapendwa wangu;
giza limekuwa ndilo rafiki yangu wa karibu kuliko wote.

*Zaburi 88:3 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.

Zaburi 88:11 Yaani Abadon.