Zaburi 89
Wimbo Wakati Wa Taabu Ya Kitaifa
Utenzi wa Ethani Mwezrahi.
1 Nitaimba juu ya upendo mkuu wa Bwana milele;
kwa kinywa changu nitajulisha uaminifu wako
ujulikane kwa vizazi vyote.
2 Nitatangaza kuwa upendo wako unasimama imara milele
na uaminifu wako umeuthibitisha mbinguni.
3 Ulisema, “Nimefanya agano na mteule wangu,
nimemwapia mtumishi wangu Daudi,
4 ‘Nitaimarisha uzao wako milele
na kudumisha ufalme wako kwa vizazi vyote.’ ”
5 Ee Bwana, mbingu zinayasifu maajabu yako,
uaminifu wako pia katika kusanyiko la watakatifu.
6 Kwa kuwa ni nani katika mbingu
anayeweza kulinganishwa na Bwana?
Ni nani miongoni mwa viumbe vya mbinguni
aliye kama Bwana?
7 Katika kusanyiko la watakatifu, Mungu huogopwa sana,
anahofiwa kuliko wote wanaomzunguka.
8 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
ni nani aliye kama wewe?
Ee Bwana, wewe ni mwenye nguvu,
na uaminifu wako unakuzunguka.
9 Wewe unatawala bahari yenye msukosuko;
wakati mawimbi yake yanapoinuka, wewe unayatuliza.
10 Wewe ulimponda Rahabu* Rahabu hapa ina maana jina la Misri kwa fumbo, yaani mwenye majivuno (lakini sio Rahabu wa Yos 2).
kama mmojawapo wa waliochinjwa;
kwa mkono wako wenye nguvu,
uliwatawanya adui zako.
11 Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako,
uliuwekea ulimwengu msingi
pamoja na vyote vilivyomo.
12 Uliumba kaskazini na kusini;
Tabori na Hermoni wanaliimbia jina lako kwa furaha.
13 Mkono wako umejaa uwezo;
mkono wako una nguvu,
mkono wako wa kuume umetukuzwa.
14 Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako cha enzi;
upendo na uaminifu vinakutangulia.
15 Heri ni wale ambao wamejifunza kukusifu kwa shangwe,
wanaotembea katika mwanga
wa uwepo wako, Ee Bwana.
16 Wanashangilia katika jina lako mchana kutwa,
wanafurahi katika haki yako.
17 Kwa kuwa wewe ni utukufu na nguvu yao,
kwa wema wako unatukuza pembe† Pembe inawakilisha nguvu. yetu.
18 Naam, ngao yetu ni mali ya Bwana,
na mfalme wetu mali ya Aliye Mtakatifu wa Israeli.
19 Ulizungumza wakati fulani katika maono,
kwa watu wako waaminifu, ukasema:
“Nimeweka nguvu kwa shujaa,
nimemwinua kijana miongoni mwa watu.
20 Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,
na nimemtia mafuta yangu matakatifu.
21 Kitanga changu kitamtegemeza,
hakika mkono wangu utamtia nguvu.
22 Hakuna adui atakayemtoza ushuru,
hakuna mtu mwovu atakayemwonea.
23 Nitawaponda adui zake mbele zake
na kuwaangamiza watesi wake.
24 Upendo wangu mkamilifu utakuwa pamoja naye,
kwa Jina langu pembe yake itatukuzwa.
25 Nitauweka mkono wake juu ya bahari,
mkono wake wa kuume juu ya mito.
26 Naye ataniita kwa sauti, ‘Wewe ni Baba yangu,
Mungu wangu, Mwamba na Mwokozi wangu.’
27 Nitamteua pia awe mzaliwa wangu wa kwanza,
aliyetukuka kuliko wafalme wote wa dunia.
28 Nitadumisha upendo wangu kwake milele,
na agano langu naye litakuwa imara.
29 Nitaudumisha uzao wake milele,
kiti chake cha enzi kama mbingu zinavyodumu.
30 “Kama wanae wataacha amri yangu
na wasifuate sheria zangu,
31 kama wakihalifu maagizo yangu
na kutoshika amri zangu,
32 nitaadhibu dhambi yao kwa fimbo,
uovu wao kwa kuwapiga,
33 lakini sitauondoa upendo wangu kwake,
wala sitausaliti uaminifu wangu kamwe.
34 Mimi sitavunja agano langu
wala sitabadili lile ambalo midomo yangu imelitamka.
35 Mara moja na kwa milele, nimeapa kwa utakatifu wangu,
nami sitamdanganya Daudi:
36 kwamba uzao wake utaendelea milele,
na kiti chake cha enzi kitadumu mbele zangu kama jua;
37 kitaimarishwa milele kama mwezi,
shahidi mwaminifu angani.”
38 Lakini wewe umemkataa, umemdharau,
umemkasirikia sana mpakwa mafuta wako.
39 Umelikana agano lako na mtumishi wako,
na umeinajisi taji yake mavumbini.
40 Umebomoa kuta zake zote,
na ngome zake zote umezifanya kuwa magofu.
41 Wote wapitao karibu wamemnyangʼanya mali zake;
amekuwa dharau kwa jirani zake.
42 Umeutukuza mkono wa kuume wa adui zake,
umewafanya watesi wake wote washangilie.
43 Umegeuza makali ya upanga wake,
na hukumpa msaada katika vita.
44 Umeikomesha fahari yake,
na kukiangusha kiti chake cha enzi.
45 Umezifupisha siku za ujana wake,
umemfunika kwa vazi la aibu.
46 Hata lini, Ee Bwana? Utajificha milele?
Ghadhabu yako itawaka kama moto hata lini?
47 Kumbuka jinsi maisha yangu yanavyopita haraka.
Ni kwa ubatili kiasi gani umemuumba mwanadamu!
48 Ni mtu gani awezaye kuishi na asione kifo,
au kujiokoa mwenyewe kutoka nguvu za kaburi?‡ Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.
49 Ee Bwana, uko wapi upendo wako mkuu wa mwanzoni,
ambao katika uaminifu wako ulimwapia Daudi?
50 Bwana kumbuka jinsi mtumishi wako amesimangwa,
jinsi ninavyovumilia moyoni mwangu dhihaka za mataifa yote,
51 dhihaka ambazo kwazo adui zako
wamenisimanga, Ee Bwana,
ambazo kwazo wamesimanga
kila hatua ya mpakwa mafuta wako.
52 Msifuni Bwana milele!
Amen na Amen.
*Zaburi 89:10 Rahabu hapa ina maana jina la Misri kwa fumbo, yaani mwenye majivuno (lakini sio Rahabu wa Yos 2).
†Zaburi 89:17 Pembe inawakilisha nguvu.
‡Zaburi 89:48 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.