8
1 Watu wote walikusanyika kama mtu mmoja katika eneo la wazi mbele ya lango la maji. Wakamwomba Ezra mwandishi akilete Kitabu cha Sheria ya Musa, ambacho Bwana aliwaamuru Israeli. 2 Siku ya kwanza ya mwezi wa saba, Ezra, kuhani, akaleta sheria mbele ya mkutano, wanaume na wanawake, na wote waliokuwa na uwezo wa kusikia na kuelewa. 3 Akatizama eneo lililo wazi mbele ya lango la Maji, na akasoma toka asubuhi hadi adhuhuri, mbele ya wanaume na wanawake, na yeyote ambaye angeweza kuelewa. Na wote wakasikiliza kwa makini kitabu cha Sheria. 4 Na Ezra, mwandishi, alisimama juu ya jukwaa la mbao ambalo watu walikuwa wametengeneza kwa kusudi hilo. Pembeni yake walisimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya, upande wake wa kuume; na Pedaya, Misbaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadani, Zekaria na Meshulamu walikuwa wamesimama upande wake wa kushoto. 5 Ezra alifungua kitabu mbele ya watu wote, kwa kuwa alikuwa amesimama juu ya watu, na alipoufungua watu wote wakasimama. 6 Ezra akamshukuru Bwana, Mungu mkuu; na watu wote wakainua mikono yao, wakajibu, “Amina! Amina!” Wakainamisha vichwa vyao, wakamwabudu Bwana kwa nyuso zao zikiwa chini. 7 Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodai, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabidi, Hanania, Pelaya nao ni Walawi, waliwasaidia watu kuelewa sheria, watu wakakaa mahali pao. 8 Wao walisoma katika kitabu, Sheria ya Mungu, wakaeleza wazi kwa tafsiri na kutoa maana ili watu waelewe yaliyosomwa. 9 Nehemia, gavana, na Ezra kuhani, na mwandishi, na Walawi waliokuwa wakitafsiri kwa watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu. Msiomboleze au kulia. Kwa kuwa watu wote walilia wakati waliposikia maneno ya sheria. 10 Nehemia akawaambia, 'Nendeni, mle kilichonona, mkate na maji ya kunywa, na mpelekeni mtu asiye na kitu, kwa maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu. Msiwe na huzuni, kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu. 11 Basi Walawi wakawafanya watu kuwa na utulivu, wakisema, “Nyamazeni! kwa maana siku hii ni takatifu. Msiwe na huzuni.” 12 Watu wote wakaenda kula na kunywa na kugawana chakula na kusherehekea kwa furaha kubwa kwa sababu walielewa maneno waliyohubiriwa. 13 Siku ya pili viongozi wa nyumba za mababu kutoka kwa watu wote, makuhani na Walawi, wakakusanyika kwa Ezra, mwandishi ili kupata ufahamu kutoka kwenye maneno ya sheria. 14 Wakaona imeandikwa katika sheria namna Bwana alivyomuamuru Musa kwamba wana wa Israeli waishi katika hema wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba. 15 Wanapaswa kutoa tamko katika miji yao yote, na huko Yerusalemu, wakisema, 'Nendeni nje kwenye nchi ya vilima, na mkalete matawi kutoka kwenye mzeituni mwitu, na matawi ya mihadsi, na matawi ya mitende na matawi ya miti minene ili kufanya vibanda vya muda kama ilivyoandikwa.” 16 Basi watu wakatoka na kuleta matawi, wakajifanyia mahema, kila mmoja juu ya paa zao, katika ua zao, katika mahakama za nyumba ya Mungu, mahali pa wazi pa lango la Maji, na katika mraba wa lango la Efraimu. 17 Kisha kusanyiko lote la wale waliorudi kutoka kifungoni wakafanya mahema na kukaa ndani yake. Kwa kuwa tangu siku za Yoshua, mwana wa Nuni hata siku hiyo, watu wa Israeli hawakuadhimisha sikukuu hii. Na furaha ilikuwa kubwa sana. 18 Pia siku kwa siku, tangu siku ya kwanza hadi mwisho, Ezra alisoma kutoka Kitabu cha Sheria ya Mungu. Walifanya sikukuu kwa siku saba na siku ya nane kilikuwa na kusanyiko zuri, kwa utiifu wa amri.