11
1 Nilipewa mwanzi wa kutumia kama fimbo ya kupimia. Niliambiwa, “Ondoka na ukapime hekalu la Mungu na madhabahu, na wale wanaoabudu ndani yake. 2 Lakini usipime eneo la ua wa nje ya hekalu, kwa kuwa wamepewa watu wa Mataifa. Wataukanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili. 3 Nitawapa mashahidi wangu wawili mamlaka ya kutabiri kwa muda wa siku 1, 260, wakiwa wamevaa magunia.” 4 Hawa mashahidi ni miti miwili ya mizeituni na vinara viwili ambavyo vimesimama mbele ya Bwana wa dunia. 5 Kama mtu yeyote ataamua kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwadhuru adui zao. Yeyote anayetaka kuwadhuru lazima auawe kwa njia hii. 6 Hawa mashahidi wana uwezo wa kufunga anga ili kwamba mvua isinyeshe wakati wanatabiri. Wana nguvu ya kubadili maji kuwa damu na kuipiga nchi kwa kila aina ya pigo wakati wowote wakitaka. 7 Wakati watakapokuwa wamemaliza ushuhuda wao, yule mnyama anayetoka kwenye shimo lisilo na mwisho atafanya vita dhidi yao. Atawashinda na kuwaua. 8 Miili yao italala katika mtaa wa mji mkuu (ambao kimfano unaitwa Sodoma na Misri) ambapo Bwana wao alisulubiwa. 9 Kwa siku tatu na nusu baadhi kutoka katika jamaa za watu, kabila, lugha na kila taifa watatazama miili yao na hawatatoa kibali kuwekwa katika kaburi. 10 Wale wanaoishi katika nchi watafurahi kwa ajili yao na kushangilia, hata kutumiana zawadi kwa sababu hao manabii wawili waliwatesa wale walioishi katika nchi. 11 Lakini baada ya siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu itawaingia nao watasimama kwa miguu yao. Hofu kuu itawaangukia wale wanaowaona. 12 Kisha watasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njoni huku!” Nao watakwenda juu mbinguni katika wingu, wakati adui zao wakitazama. 13 Katika saa hiyo kutakuwepo na tetemeko kuu la ardhi na moja ya kumi ya mji itaanguka. Watu elfu saba watauawa katika tetemeko na watakaobaki hai wataogopeshwa na kumpa utukufu Mungu wa mbinguni. 14 Ole ya pili imepita. Angalia! Ole ya tatu inakuja upesi. 15 Kisha malaika wa saba alipiga tarumbeta yake, na sauti kubwa zilinena mbinguni na kusema, “Ufalme wa dunia umeshakuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake. Atatawala milele na milele.” 16 Kisha wazee ishirini na wanne waliokuwa wameketi kwenye viti vya enzi mbele ya Mungu walianguka wenyewe chini kwenye ardhi, nyuso zao zimeinama chini, nao walimwabudu Mungu. 17 Walisema, “Twatoa shukrani zetu kwako, Bwana Mungu, mtawala juu ya vyote, ambaye upo na ambaye ulikuwepo, kwa sababu umetwaa nguvu yako kuu na kuanza kutawala. 18 Mataifa walikasirika, lakini gadhabu yako imekuja. Wakati umefika kwa wafu kuhukumiwa na wewe kuwazawadia watumishi wako manabii, waamini na wale walio na hofu ya jina lako, wote wawili wasiofaa kitu na wenye nguvu. Na wakati wako umefika wa kuwaharibu wale ambao wamekuwa wakiiharibu dunia.” 19 Kisha hekalu la Mungu mbinguni lilifunuliwa na sanduku la agano lake lilionekana ndani ya hekalu lake. Kulikuwa na miali ya mwanga, kelele, ngurumo za radi, tetemeko la ardhi na mawe ya mvua.