12
1 Ishara kuu ilionekana mbinguni: mwanamke aliyefunikwa na jua, na akiwa na mwezi chini ya miguu yake; na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa juu ya kichwa chake. 2 Alikuwa na mimba na alikuwa analia kwa ajili ya maumivu ya kuzaa—katika uchungu wa kujifungua. 3 Na ishara nyingine ilionekana mbinguni: Tazama! Kulikuwa na joka mwekundu mkubwa ambaye alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na kulikuwa na taji saba kwenye vichwa vyake. 4 Mkia wake ulikokota theluthi moja ya nyota mbinguni na kuzitupa chini duniani. Joka alisimama mbele ya mwanamke aliyekuwa anakaribia kuzaa, ili kwamba wakati anazaa, apate kummeza mtoto wake. 5 Alimzaa mwana, mtoto wa kiume, ambaye atayatawala mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Mtoto wake alinyakuliwa juu kwa Mungu na kwenye kiti chake cha enzi, 6 na mwanamke alikimbilia nyikani, mahali ambapo Mungu alikuwa ameandaa eneo kwa ajili yake, ili aweze kuhudumiwa kwa siku 1, 260. 7 Sasa kulikuwa na vita mbinguni. Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka; naye joka mkubwa na malaika zake wakapigana nao. 8 Lakini joka hakuwa na nguvu za kutosha kushinda. Kwa hiyo haikuwepo tena nafasi mbinguni kwa ajili yake na malaika zake. 9 Joka mkubwa—yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani ambaye hudanganya - dunia nzima akatupwa chini katika dunia, na malaika zake wakatupwa chini pamoja naye. 10 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni: “Sasa wokovu umekuja, nguvu—na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake. Kwa kuwa mshitaki wa ndugu zetu ametupwa chini—ambaye aliwashitaki mbele za Mungu wetu mchana na usiku. 11 Walimshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wao, kwa maana hawakupenda sana maisha yao, hata kufa. 12 Kwa hiyo, shangilieni, ninyi mbingu, na wote mnaokaa ndani yake. Lakini ole wa nchi na bahari kwa sababu mwovu ameshuka kwenu. Amejawa na hasira kali, kwa sababu anajua kwamba ana muda mchache tu. 13 Wakati joka alipotambua kuwa ametupwa chini kwenye nchi, alimfuata mwanamke ambaye alikuwa amezaa mtoto wa kiume. 14 Lakini mwanamke alipewa mabawa mawili ya tai mkubwa, ili kwamba aweze kuruka hadi kwenye eneo lililoandaliwa kwa ajili yake kule jangwani, eneo ambalo angeweza kutunzwa, kwa wakati, nyakati na nusu wakati-mahali asipoweza kupafikia huyo nyoka. 15 Nyoka alimwaga maji kutoka mdomoni mwake kama mto, ili afanye gharika ya kumgharikisha. 16 Lakini ardhi ilimsaidia mwanamke. Ilifunua kinywa chake na kuumeza mto alioutema joka kutoka kinywani mwake. 17 Kisha joka akamkasirikia mwanamke naye aliondoka na kufanya vita na uzao wake wote—wale wanaotii amri za Mungu na kushikilia ushuhuda kuhusu Yesu. 18 Kisha joka alisimama juu ya mchanga ufukwe wa bahari.